Serikali ya Tanzania imesisitiza msimamo wake wa kutoruhusu mahusiano ya kimapenzi ya watu wa jinsia moja.

Aidha imekataa mapendekezo ya kimataifa yaliyotaka nchi hiyo kuondoa sheria zinazoharamisha mahusiano hayo.

Msimamo huo umetangazwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Abdallah Ulega, wakati akiwasilisha majibu ya Serikali kuhusu mapendekezo yaliyotolewa na mataifa mbalimbali katika tathmini ya hali ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa (UPR), iliyofanyika mjini Geneva, Uswisi.

Katika tathmini hiyo, Tanzania imekataa jumla ya mapendekezo 68 kati ya 280 yaliyowasilishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, huku ikikubali mapendekezo 196 na kuahirisha kutoa msimamo kuhusu mengine 16 kwa ajili ya uchambuzi zaidi.

Ulega amesema Serikali haijaunga mkono mapendekezo yanayotaka kuondolewa kwa adhabu zinazohusiana na makosa ya kujamiiana kinyume na maumbile, akieleza kuwa hatua hiyo inazingatia Katiba, sheria, mila, desturi na maadili ya jamii ya Kitanzania.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, Tanzania inaamini kuwa masuala yanayohusu mabadiliko ya sheria na sera za kitaifa yanapaswa kuzingatia mazingira ya kijamii na kiutamaduni ya nchi husika.

Miongoni mwa mataifa yaliyotaka Tanzania ibadili msimamo wake ni Australia, Iceland, Malta, Ecuador, Luxembourg na Hispania, ambayo yalipendekeza kuondolewa kwa vifungu vya sheria vinavyoharamisha mahusiano ya jinsia moja baina ya watu wazima wanaokubaliana.

Baadhi ya mataifa hayo pia yalitaka kuwepo kwa sheria zinazolinda watu dhidi ya ubaguzi unaotokana na mwelekeo wao wa kimapenzi, pamoja na kuhakikisha wanapata huduma za afya bila kubaguliwa.

Hata hivyo, Serikali ya Tanzania imesema haitounga mkono mapendekezo hayo kwa kuwa yanakinzana na misingi ya sheria na maadili ya jamii nchini humo.

Katika hatua nyingine, tathmini hiyo imeibua pia masuala yanayohusu mwenendo wa haki za binadamu nchini Tanzania kufuatia uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Mataifa kadhaa, yakiwemo Ujerumani, Uingereza, Finland na Uswisi, yalieleza wasiwasi kuhusu madai ya vifo, watu kupotezwa, kukamatwa kiholela na matumizi ya nguvu kupita kiasi na vyombo vya usalama.

Mataifa hayo yalitaka uchunguzi huru ufanyike kuhusu madai hayo, waliohusika wawajibishwe na waathiriwa pamoja na familia zao wapewe haki na fidia stahiki.

Kuhusu mapendekezo 16 yaliyoahirishwa, Ulega amesema Serikali inahitaji muda zaidi kufanya tathmini ya athari zake za kisheria, kisera na kiuchumi kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho.

Tanzania imeeleza kuwa itawasilisha msimamo wake kuhusu mapendekezo hayo katika kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kinachotarajiwa kufanyika Februari 2027.