Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limeitaka serikali ya Sudan kumkabidhi mara moja aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Ahmed Haroun, kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ili akabiliane na mashtaka mazito yanayohusiana na mauaji na ukiukaji wa haki za binadamu katika eneo la Darfur.

Wito huo umetolewa kufuatia kukamatwa kwa Haroun na kuwekwa chini ya ulinzi wa mamlaka za Sudan, hatua ambayo HRW inasema inapaswa kufuatiwa na kukabidhiwa kwake kwa ICC iliyoko The Hague, Uholanzi, ambako anashtakiwa kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.

Mashtaka yanayomkabili Haroun yanahusiana na matukio yaliyotekelezwa katika eneo la Darfur magharibi mwa Sudan mwaka 2003 na 2004, kipindi ambacho eneo hilo lilikumbwa na mapigano makali yaliyosababisha vifo vya watu wengi, uharibifu wa makazi na kuondoka kwa maelfu ya wananchi kutoka maeneo yao.

Kwa mujibu wa HRW, Haroun alikamatwa tena Novemba 8, 2026, na Jeshi la Sudan (SAF), siku moja baada ya kushiriki mahojiano katika kipindi cha mazungumzo ya video (podcast), ambayo yalikuwa mara yake ya kwanza kuonekana hadharani tangu mwaka 2019.

Hata hivyo, jeshi la Sudan halijathibitisha rasmi mahali anapozuiliwa, ingawa taarifa za vyombo vya habari zinaeleza kuwa huenda anashikiliwa katika jimbo la Khartoum.

Mahakama ya ICC ilitoa hati ya kumkamata Haroun mwaka 2007, ikimtuhumu kwa makosa 20 ya uhalifu dhidi ya binadamu na makosa 22 ya uhalifu wa kivita yaliyodaiwa kutekelezwa Darfur.

Katika kipindi hicho, vikosi vya serikali ya Sudan pamoja na wanamgambo waliokuwa washirika wake vilituhumiwa kufanya mashambulizi yaliyolenga raia kwa misingi ya makabila, yakiwemo mauaji, ubakaji, kuwafurusha watu kwa lazima kutoka makazi yao na kuchoma vijiji.

Mkurugenzi wa masuala ya haki za kimataifa wa HRW, Liz Evenson, amesema waathiriwa wa ukatili wa Darfur wamekuwa wakisubiri haki kwa takribani miongo miwili huku washukiwa wakikwepa mkono wa sheria.

Evenson amesema kukabidhiwa kwa washukiwa hao kwa mahakama ya The Hague kutatoa ujumbe mzito kwa watu wanaotekeleza uhalifu nchini Sudan kwa sasa kwamba nao wanaweza kufikishwa mahakamani.

HRW pia imetaka serikali ya Sudan kumkabidhi aliyekuwa Rais Omar al-Bashir, ambaye inaamini anashikiliwa katika jimbo la Khartoum, pamoja na kumtafuta, kumkamata na kumkabidhi aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Abdelrahim Mohamed Hussein, ambaye alipo kwa sasa hakujulikani.

Al-Bashir anakabiliwa na hati mbili za kukamatwa zilizotolewa na ICC mwaka 2009 na 2010, zikimhusisha na uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu na mauaji ya kimbari yaliyodaiwa kutekelezwa Darfur kati ya 2003 na 2008.

HRW imesema Sudan ina wajibu wa kushirikiana na ICC chini ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nambari 1593, licha ya nchi hiyo kutokuwa mwanachama wa mkataba wa Roma ulioanzisha mahakama hiyo.

Shirika hilo sasa linaitaka Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na mataifa yenye ushawishi kuitaka Sudan kutekeleza wajibu huo na kuhakikisha washukiwa wote wanaotafutwa na ICC wanafikishwa mbele ya mahakama kujibu mashtaka yanayowakabili.