Shirikisho la Soka Afrika (CAF) linazingatia kurejea kwa mfumo wa kuandaa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kila baada ya miaka miwili, miezi michache tu baada ya kutangaza mabadiliko yaliyolenga kufanya mashindano hayo yafanyike kila baada ya miaka minne.
Rais wa CAF, Patrice Motsepe, anaripotiwa kueleza kuwa shirikisho hilo linatathmini upya mpango huo, ambao ulikuwa umepangwa kuanza kutekelezwa baada ya mashindano ya mwaka 2027 yatakayoandaliwa kwa pamoja na Kenya, Uganda na Tanzania.
Hatua hiyo inazua maswali kuhusu mustakabali wa ratiba ya mashindano makubwa zaidi ya soka barani Afrika, ambayo kwa miongo kadhaa yamekuwa yakifanyika kila baada ya miaka miwili tangu kuanzishwa kwake mwaka 1957.
Mpango wa awali wa kubadilisha ratiba ulitangazwa Desemba 2025, huku CAF ikieleza kuwa AFCON ingeanza kufanyika kila baada ya miaka minne kuanzia 2028.
Mabadiliko hayo yalihusishwa na juhudi za kuratibu vyema mashindano ya kimataifa, kupunguza migongano ya ratiba na ligi za soka barani Ulaya na kuimarisha mapato ya soka la Afrika.
CAF pia ilikuwa imependekeza kuanzishwa kwa African Nations League kuanzia mwaka 2029, mashindano ambayo yangewapa timu za taifa fursa ya kucheza mechi za ushindani kila mwaka.
Hata hivyo, kurejea kwa mfumo wa miaka miwili kungehitaji CAF kutathmini upya namna mashindano yake yanavyopangwa na jinsi yanavyoweza kuendana na kalenda ya kimataifa ya soka.
AFCON ni chanzo muhimu cha mapato kwa CAF na mashirikisho ya soka ya nchi wanachama, huku mashindano hayo yakitoa jukwaa kwa wachezaji wa Afrika kuonyesha vipaji vyao mbele ya mashabiki duniani.
Kwa upande mwingine, mfumo wa sasa umekuwa ukikabiliwa na changamoto za kupanga tarehe za mashindano kutokana na msongamano wa ratiba za klabu na timu za taifa.
Klabu nyingi za Ulaya zimekuwa zikieleza wasiwasi kuhusu kuwakosa wachezaji wao wa Kiafrika wakati wa AFCON, hasa mashindano yanapofanyika katikati ya msimu wa ligi.
AFCON ya mwaka 2027 inatarajiwa kuandaliwa na Kenya, Uganda na Tanzania, ikiwa ni mara ya kwanza kwa nchi tatu za Afrika Mashariki kushirikiana kuandaa mashindano hayo.
Iwapo CAF itaamua kurejea rasmi kwenye mfumo wa miaka miwili, uamuzi huo utakuwa na athari kubwa kwa mipango ya mashindano yajayo, mapato ya shirikisho na maandalizi ya nchi zitakazopangiwa kuwa wenyeji.
Hata hivyo, tathmini ya mpango huo haimaanishi kuwa CAF tayari imebatilisha rasmi uamuzi wake wa awali.









