Nyota wa soka kutoka Ureno, Cristiano Ronaldo, ameibuka mshindi wa tuzo ya B.O.A.T. (Ballon d’Or of All Time), baada ya mashabiki kumchagua kuwa na msimu bora zaidi miongoni mwa washindi wa tuzo ya Ballon d’Or katika historia ya soka.
Ronaldo aliibuka mshindi kupitia msimu wake wa 2008 akiwa na Manchester United, akimzidi mpinzani wake wa muda mrefu Lionel Messi, ambaye msimu wake wa 2012 ulishika nafasi ya pili katika kura hizo zilizoandaliwa na jarida la France Football.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 41 alitumia msimu wa 2007/08 kuonyesha ubora wake, akifunga mabao 42 katika mashindano yote na kuisaidia Manchester United kutwaa mataji ya Ligi Kuu ya Uingereza na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mafanikio hayo yalichangia Ronaldo kushinda Ballon d’Or yake ya kwanza mwaka 2008, kabla ya kuongeza mataji mengine manne mwaka 2013, 2014, 2016 na 2017.
Katika matokeo ya mwisho ya kura hizo, Messi alimaliza nafasi ya pili kupitia msimu wake wa 2012, wakati Ronaldo alishika nafasi ya tatu kupitia msimu wake wa 2017 akiwa Real Madrid.
Ushindi huo unampa Ronaldo nafasi ya kipekee katika kura za mashabiki, ingawa hauongezi idadi ya tuzo zake rasmi za Ballon d’Or, ambazo bado ni tano, dhidi ya nane za Messi.
Baada ya kutangazwa mshindi, Ronaldo aliwashukuru mashabiki wake kupitia mitandao ya kijamii, akisisitiza kuwa soka ni mali ya mashabiki.
“Football belongs to the fans! Thank you to all the fans around the world. Ballon d’Or of All Time is also yours,” aliandika Ronaldo.
Tuzo ya B.O.A.T. ilianzishwa kama sehemu ya kutambua historia ya Ballon d’Or, huku mashabiki wakipewa nafasi ya kuchagua msimu bora zaidi kati ya wachezaji waliowahi kushinda tuzo hiyo mara mbili au zaidi.
Tofauti na Ballon d’Or ya kawaida, ambayo huamuliwa kwa utaratibu wa upigaji kura wa waandishi wa habari, mshindi wa B.O.A.T. aliamuliwa na mashabiki kupitia kura za mtandaoni.
Hata hivyo, tuzo hiyo ni ya heshima na haichukuliwi kama Ballon d’Or nyingine rasmi.
Ushindani kati ya Ronaldo na Messi umeendelea kuwa mojawapo ya mijadala mikubwa katika soka la dunia, huku nyota hao wawili wakitawala tuzo za kibinafsi kwa takriban miongo miwili.









