Sakata la kutoweka kwa mwanaharakati wa Tanzania Twaha Mwaipaya limezidi kuvuta hisia za umma katika eneo la Afrika Mashariki, huku maswali kuhusu usalama wake yakizidi kuikumba serikali ya Kenya na vyombo vyake vya usalama.
Mawakili wa Vocal Africa, wakiongozwa na Martha Karua, wameiomba Mahakama Kuu kuamuru Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Mohamed Amin kufika wenyewe mahakamani kueleza aliko Mwaipaya.
Karua alisema vyombo vya usalama vilikuwa na taarifa kuhusu kutoweka kwa mwanaharakati huyo tangu Jumapili, siku ambayo tukio hilo liliripotiwa, na hivyo havipaswi kujitetea kwa madai kwamba vilipokea rasmi amri za mahakama Ijumaa.
Alisisitiza kuwa taarifa kuhusu kutoweka kwa Mwaipaya ziliripotiwa pia na vyombo vya habari, hali ambayo ilipaswa kuchochea hatua za haraka za uchunguzi na utafutaji.
“Ni jukumu la polisi na vyombo vya usalama kuhakikisha usalama wa kila mtu. Hawawezi kusema walianza uchunguzi Ijumaa ilhali walikuwa wamejulishwa tangu Jumapili,” Karua aliambia mahakama.
Wakili huyo alionya kuwa tukio hilo halipaswi kuchukuliwa kama kesi ya kawaida, akitaja visa vingine vya watu kutoweka na kutekwa nyara katika eneo la Afrika Mashariki vilivyofikishwa mahakamani kati ya Desemba 2024 na 2025.
Alisema baadhi ya watu waliotoweka walipatikana wakiwa hai huku wengine wakipatikana wamefariki, akitaka vyombo vya usalama viwe na uwezo wa kuchukua hatua kwa wakati.
Karua pia alipinga hatua ya kuwatuma maafisa wawili wa ngazi za chini mahakamani, akisema haikidhi uzito wa maswali yanayoulizwa na Wakenya, Watanzania na Waganda wanaofuatilia kesi hiyo.
Alitaka Kanja na Amin wafike wenyewe kutoa maelezo kuhusu hatua zilizochukuliwa kumtafuta Mwaipaya, akisisitiza kuwa mamlaka yao ndiyo inayoweza kutoa majibu yanayotarajiwa.
Karua alidai kuwa polisi tayari wamekiuka amri ya pili ya mahakama iliyowataka kumwasilisha Mwaipaya mbele ya mahakama.
“Bado hatuna Mwaipaya hapa wala mwili wake. Waje wajibu maswali ya Wakenya, Watanzania na Waganda,” alisema, akiongeza kuwa serikali inataka kumrejesha mwanaharakati huyo katika nchi aliyokimbia.
Hata hivyo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilipinga ombi la kuwaita wakuu hao wa polisi, ikisema kuwa uchunguzi kuhusu kutoweka kwa Mwaipaya unaendelea.
Wakili wa serikali Marwa aliomba mahakama itoe mamlaka muda wa kuwasilisha matokeo ya uchunguzi, akisema hatua zaidi zinaweza kuchukuliwa iwapo mahakama haitaridhishwa na majibu yatakayotolewa.
Jaji Muteti anatarajiwa kutoa maelekezo kuhusu iwapo Kanja na Amin watahitajika kufika mahakamani binafsi, hatua inayoweza kuamua mwelekeo wa kesi hiyo inayofuatiliwa kwa karibu katika eneo la Afrika Mashariki.









