Watano Wakamatwa Baada Ya Mkulima Kupigwa Risasi Na Kuteswa Afrika Kusini

Polisi nchini Afrika Kusini wamewakamata washukiwa watano kuhusiana na shambulizi la kikatili dhidi ya mkulima mwenye umri wa miaka 50, aliyepigwa risasi, kuchomwa visu na kuteswa kabla ya washambuliaji kumkata masikio yote mawili katika shamba lake.

Washukiwa hao walikamatwa kufuatia uchunguzi wa kina uliofanywa na maafisa wa polisi baada ya tukio hilo lililotokea Jumatano, Oktoba 28, katika eneo la Syferfontein, karibu na Ventersdorp, jimbo la North West.

Kwa mujibu wa taarifa za polisi, waathiriwa katika shambulizi hilo ni mkulima Donovan Marx, ambaye alishambuliwa na watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki baada ya kuvamia shamba lake.

Inaripotiwa kuwa washambuliaji watatu waliingia katika shamba hilo na kumkabili mfanyakazi mmoja, ambaye walimfunga mikono na miguu kwa kutumia vifaa vya plastiki kabla ya kumhoji kuhusu mahali alikokuwa mwajiri wake.

Hali ilizidi kuwa mbaya pale Marx alipowasili katika eneo hilo kwa gari lake aina ya Isuzu, ambapo washambuliaji walimpiga risasi sehemu ya juu ya mwili kabla ya kumvuta ndani ya nyumba na kuendelea kumshambulia.

Mkulima huyo alidungwa visu, kupigwa na kuteswa, huku washambuliaji wakimkata masikio yote mawili.

Baadaye walivamia nyumba yake, wakachukua bunduki tatu kutoka kwenye kabati la kuhifadhia silaha na kutoroka kwa kutumia gari lake.

Polisi walisema washukiwa wawili walikamatwa Jumamosi, Oktoba 31, katika eneo la Ventersdorp, kabla ya wengine watatu kunaswa Jumapili, Novemba 1, katika eneo la Promosa, karibu na Potchefstroom.

Operesheni hiyo iliongozwa na wapelelezi wa Ventersdorp wakishirikiana na kikosi maalumu cha kupambana na magenge ya uhalifu.

Wakati wa operesheni hiyo, maafisa walikamata bunduki nne, ambapo mbili kati yake zimehusishwa na shambulizi hilo.

Pia walipata nguo na vito vya thamani vinavyohusishwa na uchunguzi.

Washukiwa hao watano, wenye umri wa kati ya miaka 26 na 56, wanatarajiwa kufikishwa katika mahakama za Ventersdorp na Potchefstroom Jumanne, Novemba 3, kujibu mashtaka ya wizi wa kutumia nguvu nyumbani, jaribio la mauaji na kumiliki silaha pamoja na risasi kinyume cha sheria.