Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi wapya wa Tume za Haki za Binadamu na Utawala Bora kuwa makini kufuatilia mwenendo wa haki za binadamu ndani na nje ya nchi, huku akisisitiza umuhimu wa kutoa majibu ya haraka kuhusu shutuma zinazoelekezwa dhidi ya serikali yake.
Kauli ya Samia inajiri wakati Tanzania ikiendelea kukabiliwa na shinikizo la ndani na kimataifa kuhusu masuala ya haki za binadamu kufuatia ghasia zilizoshuhudiwa baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, zilizoripotiwa kusababisha vifo, majeruhi na madai ya ukiukaji wa haki za raia.
Akizungumza Jumatatu, Novemba 2, 2026, katika hafla ya kuwaapisha viongozi hao Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma, Samia alisema mazingira ya sasa ya kimataifa yanahitaji taasisi zinazohusika na haki za binadamu kuwa tayari kuchunguza taarifa na kujibu hoja zinazotolewa dhidi ya nchi.
Alisema ni muhimu kwa tume hiyo kufuatilia kile kinachozungumzwa kuhusu Tanzania katika majukwaa ya kimataifa, kulinganisha madai hayo na hali halisi nchini na kutoa ufafanuzi kwa wakati unaofaa.
“Nataka niwaambie katika dunia ya leo, mambo yapo juu chini. Mwenye haki, ataambiwa huna haki na asiyekuwa na haki, anaambiwa ana haki,” alisema Samia.
Aliongeza kuwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inapaswa kutambua shutuma zinazoikabili Tanzania na kuhakikisha inazijibu kwa haraka.
“Hii Tume ya Haki na Utawala Bora, ili kuwa na utawala bora, lazima muone tunashutumiwa na nini nje, na hali ndani ikoje na mjibu kwa haraka,” alisema rais huyo.
Kauli hiyo inakuja takribani mwaka mmoja baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, ambao ulifuatiwa na maandamano na machafuko katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, huku masuala ya matumizi ya nguvu na vyombo vya usalama yakiendelea kujadiliwa ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa taarifa ya tume ya uchunguzi iliyowasilishwa kwa Rais Samia Aprili 2026, watu wasiopungua 518 walifariki kutokana na sababu zisizo za kawaida wakati wa machafuko hayo, ingawa ripoti hiyo haikubaini rasmi uwajibikaji wa watu binafsi kuhusu vifo hivyo.
Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu, yakiwemo Amnesty International na Human Rights Watch, yameendelea kuitaka serikali ya Tanzania kuhakikisha madai ya matumizi ya nguvu kupita kiasi, watu kupotea na kukamatwa kiholela yanafanyiwa uchunguzi huru na wa uwazi.
Amnesty International pia imesema ripoti ya awali ya tume ya uchunguzi wa machafuko hayo bado haijawekwa wazi kwa umma, jambo ambalo limeongeza wito wa uwajibikaji na uwazi katika kushughulikia malalamiko ya waathiriwa na familia zao.
Hata hivyo, serikali ya Tanzania imekuwa ikisisitiza umuhimu wa kurejesha amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa, huku ikiendeleza michakato mbalimbali ya kuchunguza mazingira yaliyochangia machafuko hayo.
Katika mazingira hayo, matarajio yanaelekezwa kwa viongozi wapya wa tume hiyo kuhakikisha taasisi wanazoziongoza zinatimiza wajibu wake wa kulinda haki za wananchi, kusikiliza malalamiko na kusimamia misingi ya utawala bora.
Wito wa Samia kwa viongozi hao unafungua mjadala kuhusu nafasi ya taasisi za haki za binadamu katika kujenga upya imani ya wananchi na kukabiliana na ukosoaji wa kimataifa wakati Tanzania ikiendelea kutafuta maridhiano baada ya kipindi cha machafuko ya kisiasa.









