Mahakama nchini India imewahukumu wanaume watatu Waislamu kifungo cha maisha gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kuchinja ng'ombe katika jimbo la Gujarat.
Hukumu hiyo imezua mjadala kutokana na uzito wa adhabu iliyotolewa.
Watatu hao, waliotambuliwa kama Vasim Qureshi, Mohammad Rafiq Qureshi na Asfaq Bahelim, pia wamepigwa faini ya rupia laki tatu za India kila mmoja, sawa na zaidi ya KSh450,000.
Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama ya Kalol katika Wilaya ya Gandhinagar, ambapo Jaji wa Mahakama ya Ziada ya Vikao, BR Rajput, alisema ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka ulithibitisha kuhusika kwa washtakiwa katika kosa hilo.
Kesi hiyo inahusiana na tukio la Agosti 22, 2024, ambapo polisi walifanya msako katika nyumba moja katika kijiji cha Jamla na kupata takriban kilo 277 za nyama iliyothibitishwa kuwa ya ng'ombe.
Maafisa wa polisi pia walipata vifaa vinavyodaiwa kutumika katika shughuli za kuchinja mifugo pamoja na gari lililokuwa limeandaliwa kusafirisha nyama hiyo.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, washtakiwa walikuwa wakishirikiana na watu wengine kununua ng'ombe waliokuwa wazee au wasiotoa maziwa kwa bei ya chini, kabla ya kuwachinja kwa lengo la kuuza nyama na kupata faida.
Watu sita walikamatwa kuhusiana na tukio hilo, lakini watatu pekee ndio waliopatikana na hatia baada ya kusikilizwa kwa kesi hiyo. Mmoja wa washukiwa alifariki dunia wakati kesi ikiendelea, huku wengine wawili wakiachiliwa huru kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha.
Katika uamuzi wake, jaji alitumia sehemu kubwa ya hukumu kueleza umuhimu wa ng'ombe katika imani na tamaduni za Kihindu, akirejelea vitabu vya kidini vya Vedas na Manusmriti.
Mahakama ilieleza kuwa ng'ombe anachukuliwa na baadhi ya waumini wa Kihindu kama mama wa ulimwengu na alama muhimu ya maisha na ustawi wa jamii.
Jaji pia alitaja imani za kale za Kihindu zinazohusisha ng'ombe na uwepo wa miungu, akisisitiza umuhimu wa kulinda mnyama huyo kwa mujibu wa sheria.
Hukumu hiyo imetolewa chini ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyama ya Gujarat ya mwaka 1954, ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2017 na kuweka kifungo cha maisha kama adhabu inayoweza kutolewa kwa kosa la kuchinja ng'ombe.
Sheria hiyo pia inaweka masharti makali kuhusu umiliki, usafirishaji, uhifadhi na uuzaji wa nyama ya ng'ombe katika jimbo hilo.
Naibu Gavana wa Gujarat, Harsh Sanghavi, amepongeza hukumu hiyo, akisema ni ujumbe kwamba serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayekiuka sheria zinazolinda ng'ombe.
Gujarat ni miongoni mwa maeneo nchini India yenye sheria kali zaidi kuhusu uchinjaji wa ng'ombe, ambao unahusishwa kwa karibu na imani za kidini za Wahindu, ambao ndio wengi nchini humo.









