Rais wa Marekani Donald Trump ameibua mjadala mpya kuhusu mustakabali wa uongozi wake baada ya kueleza kuwa angependa kuwania tena urais katika uchaguzi wa mwaka 2028, licha ya Katiba ya nchi hiyo kumwekea kizuizi cha kugombea muhula wa tatu.
Trump, ambaye kwa sasa anahudumu katika muhula wake wa pili kama rais, amesema bado anatamani kuendelea kuiongoza Marekani iwapo kungekuwa na uwezekano wa kisheria kumwezesha kuwania tena nafasi hiyo.
Akizungumzia uwezekano huo, Trump alidokeza kuwa matokeo ya kura za maoni za hivi karibuni yanaonyesha kuwa anaungwa mkono na idadi kubwa ya Wamarekani ikilinganishwa na watu wengine wanaoweza kujitokeza kuwania urais.
“Ningependa kugombea tena kama ningepata nafasi, lakini lugha ya Katiba iko wazi sana. Bado tuna zaidi ya miaka miwili, na kuna mengi yanaweza kufanyika katika kipindi hicho,” alisema Trump.
Kauli hiyo imeongeza mjadala kuhusu iwapo rais huyo anaweza kutafuta njia ya kurejea katika kinyang'anyiro cha urais, wakati muda wa muhula wake wa sasa ukiendelea kuyoyoma.
Hata hivyo, Marekebisho ya 22 ya Katiba ya Marekani yanaweka wazi kuwa hakuna mtu anayeruhusiwa kuchaguliwa kuwa rais zaidi ya mara mbili.
Kizuizi hicho kinamaanisha kuwa Trump, ambaye alichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2016 na kurejea madarakani katika uchaguzi wa 2024 baada ya kushindwa mwaka 2020, hawezi kuchaguliwa tena katika uchaguzi wa kawaida wa mwaka 2028.
Marekebisho hayo ya Katiba yaliidhinishwa mwaka 1951 kufuatia kipindi cha Rais Franklin D. Roosevelt, aliyekuwa amechaguliwa mara nne mfululizo kabla ya kufariki mwaka 1945.
Licha ya kizuizi hicho cha kikatiba, kauli za Trump zinaonyesha kuwa bado ana nia ya kuendelea kuwa sehemu muhimu ya siasa za Marekani hata baada ya kumalizika kwa muhula wake wa sasa.
Aidha, matamshi yake yanakuja wakati ambapo mjadala kuhusu mrithi wake ndani ya chama cha Republican na mwelekeo wa chama hicho katika uchaguzi ujao ukiendelea kupata uzito.
Trump anatarajiwa kumaliza muhula wake wa pili Januari 2029, huku uchaguzi mkuu wa Marekani ukipangwa kufanyika Novemba 2028.
Kwa sasa, haijabainika ni hatua gani za kisiasa au kisheria ambazo Trump anazifikiria, lakini kauli yake imefungua tena mjadala kuhusu mipaka ya mihula ya urais na mustakabali wa siasa za Marekani.









