Rais William Ruto amesema takriban Wakenya milioni 2.7 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, huku watoto na wanawake wengi wakihitaji msaada wa haraka kutokana na utapiamlo unaochochewa na ukame.
Ruto amesema ukosefu wa mvua katika maeneo kame nchini unaendelea kuhatarisha usalama wa chakula na lishe bora, hali inayozidisha changamoto za maisha kwa mamilioni ya wananchi wanaotegemea kilimo na ufugaji kujipatia riziki.
Akizungumza katika mkutano wa kilele kuhusu usalama wa chakula jijini Nairobi, Rais amesema utapiamlo unalikosesha taifa asilimia 6.9 ya pato lake la taifa, akisisitiza kuwa hali hiyo inaathiri maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa wananchi.
Amesema kukabiliana na tatizo hilo kunahitaji kuunganisha juhudi za kuongeza uzalishaji wa chakula, kuboresha lishe na kuhakikisha wananchi wanapata chakula chenye virutubisho vya kutosha.
Ruto amesema serikali inalenga kupanua mpango wa chakula shuleni kutoka wanafunzi milioni tatu wanaonufaika kwa sasa hadi milioni 10 kufikia mwaka 2030.
Mpango huo unatarajiwa kusaidia kuboresha lishe ya watoto, kuongeza mahudhurio shuleni na kupunguza mzigo wa kifedha kwa familia zinazokabiliwa na changamoto za kiuchumi.
Aidha, Rais amesema ingawa Katiba ya Kenya inatambua haki ya kila mwananchi kupata chakula cha kutosha na kuwa huru dhidi ya njaa, utekelezaji wa haki hiyo unahitaji sheria madhubuti, ufadhili wa kutosha na mifumo inayohakikisha chakula kinawafikia wananchi.
Amesisitiza kuwa usalama wa chakula haupaswi kutegemea pekee misaada ya dharura, bali unahitaji mikakati ya muda mrefu inayolenga kuimarisha uzalishaji wa ndani na uwezo wa wananchi kujikimu.
Akizungumzia hali ya kimataifa, Ruto amesema watu milioni 645 walikabiliwa na njaa mwaka 2025, huku Afrika ikiwa na watu milioni 309 wanaokumbwa na hali hiyo, sawa na mmoja kati ya kila watu watano barani humo.
Ameonya kuwa hali hiyo inatarajiwa kuwa mbaya zaidi katika miaka ijayo, huku Afrika ikitarajiwa kuchangia asilimia 60 ya watu wote watakaokabiliwa na njaa duniani kufikia mwaka 2030.
Rais amesisitiza umuhimu wa hatua za pamoja katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuongeza uzalishaji wa chakula na kuimarisha mifumo ya lishe ili kuzuia janga la njaa kuathiri zaidi wananchi.









