Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) imeonya kuhusu uwezekano wa mzozo wa kikabila unaoendelea nchini Ethiopia kuenea hadi Kenya, huku ikitoa wito wa kuimarishwa kwa kampeni za amani katika maeneo ya Kaskazini mwa nchi kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.

Tume hiyo imesema mzozo unaoendelea kati ya jamii za Oromo na Wasomali nchini Ethiopia unaweza kuhatarisha usalama na mshikamano wa jamii zinazopatikana katika kaunti za Isiolo na Marsabit, ambako jamii hizo mbili zinaishi pamoja.

Onyo hilo limetolewa kufuatia kukamilika kwa zoezi la siku tatu la kuwashirikisha wadau mbalimbali katika Kaunti ya Isiolo, lililolenga kuimarisha amani, mshikamano na utangamano wa kijamii kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Washiriki wa mkutano huo wametaka kampeni ya Uchaguzi Bila Noma kupanuliwa hadi katika ngazi za vijiji ili kuhakikisha wananchi wanadumisha amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Zoezi hilo liliwakutanisha maafisa wa serikali, wawakilishi wa mashirika ya kijamii, taasisi za kidini, watu wenye ulemavu na makundi mengine yenye maslahi maalum.

Kamishna wa NCIC, Josphine Eregae, na Katibu wa Mtandao wa Dini mbalimbali wa Isiolo, Askofu Stephen Kalunyu, walielezea wasiwasi wao kuhusu athari zinazoweza kusababishwa na mzozo huo, hasa kutokana na makumi ya maelfu ya raia wa Ethiopia kuvuka mpaka na kuingia Kenya wakitafuta hifadhi.

Viongozi hao walisisitiza umuhimu wa viongozi wa kidini kutumia majukwaa yao katika makanisa na misikiti kuhubiri amani, umoja na mshikamano miongoni mwa jamii.

Walieleza kuwa juhudi hizo ni muhimu kutokana na kuwepo kwa jamii za Oromo na Wasomali katika maeneo ya Kaskazini mwa Kenya, hali inayoweza kuongeza hatari ya mzozo huo kuathiri uhusiano wa jamii za wenyeji.

Askofu Kalunyu aliwahimiza wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kupitia mfumo wa ulinzi shirikishi na kutoa taarifa kuhusu mienendo inayoweza kuhatarisha amani na usalama.

Aidha, aliwaonya wananchi dhidi ya kuwahifadhi kiholela watu wanaokimbia kutoka katika kambi za wakimbizi za Moyale, akisema hatua hiyo inaweza kuongeza uwezekano wa mzozo huo kuenea nchini Kenya.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa serikali ya Kenya na mashirika ya kimataifa yana wajibu wa kuhakikisha wakimbizi wanaopata hifadhi nchini wanapewa uangalizi na huduma zinazohitajika hadi hali itakapokuwa salama kwao kurejea makwao.

NCIC imeendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa jamii, viongozi na vyombo vya usalama katika kuzuia migogoro na kuhakikisha uchaguzi mkuu wa 2027 unaandaliwa katika mazingira ya amani na utulivu.