Kampuni ya Amazon imepata pigo kubwa katika mpango wake wa kupanua huduma za intaneti duniani baada ya roketi iliyobeba satelaiti 40 kushindwa kutekeleza jukumu lake angani, na hivyo kuhatarisha ratiba ya kuanzisha mtandao wake mpya wa mawasiliano.
Roketi aina ya Vulcan, inayomilikiwa na kampuni ya United Launch Alliance (ULA), ilipata hitilafu takribani dakika 10 baada ya kurushwa kutoka kituo cha Cape Canaveral Space Force Station, Florida, nchini Marekani, Novemba 15, 2026.
Roketi hiyo ilikuwa imebeba satelaiti 40 za mtandao wa intaneti wa Amazon unaojulikana kama Leo, ambao kampuni hiyo inauendeleza ili kutoa huduma za intaneti kupitia satelaiti kwa maeneo mbalimbali duniani.
Hitilafu hiyo ilisababisha shehena hiyo kushindwa kufikishwa katika obiti iliyokusudiwa, huku satelaiti hizo zikiharibika na kutoweza kutekeleza jukumu lake la kutoa huduma za mawasiliano.
Tukio hilo limekuwa pigo kwa ULA, kampuni inayomilikiwa kwa ubia na Boeing pamoja na Lockheed Martin, ambayo imekuwa ikiimarisha matumizi ya Vulcan kama roketi yake kuu katika shughuli za kurusha vyombo vya anga.
Kwa kampuni hiyo, tukio hilo ni la kwanza la aina yake katika historia ya kurusha roketi, tangu kuanza kuimarisha matumizi ya Vulcan katika shughuli zake za anga.
ULA ilikuwa imepanga kutumia roketi hiyo mara kwa mara kusaidia Amazon kuweka angani mkusanyiko mkubwa wa satelaiti unaolenga kutoa huduma za intaneti kwa ushindani na mitandao mingine ya mawasiliano ya satelaiti.
Katika taarifa yake, ULA ilithibitisha kuwa roketi hiyo iliyorushwa kutoka eneo la Space Launch Complex 41 ilipata hitilafu dakika 10 baada ya kuanza safari yake na kushindwa kuwasilisha mzigo wa Amazon katika obiti ya Dunia.
Kampuni hiyo ilisema kila safari ya roketi hutoa taarifa na mafunzo muhimu kwa wahandisi, lakini kutokana na tukio hilo kuwa jipya, bado haikuwa na maelezo kamili kuhusu chanzo cha hitilafu.
Uchunguzi unatarajiwa kusaidia kubaini kilichosababisha roketi hiyo kushindwa kutekeleza jukumu lake na hatua zinazoweza kuchukuliwa kuzuia matukio kama hayo kujirudia.
Kushindwa kwa safari hiyo pia kunaweza kuathiri mipango ya Amazon ya kupanua huduma zake za intaneti, hasa ikizingatiwa kuwa kampuni hiyo inahitaji kurusha satelaiti nyingi zaidi ili kufikia malengo yake ya kimataifa.
Pamoja na changamoto hiyo, ULA na Amazon zinakabiliwa na jukumu la kubaini athari za tukio hilo kwa ratiba ya safari zijazo za roketi na maendeleo ya mtandao wa Leo.









