Polisi nchini Kenya (NPS) imeimarisha operesheni za ukaguzi wa magari na utekelezaji wa sheria za trafiki katika maeneo mbalimbali ya nchi, huku ikilenga kukabiliana na ukiukaji wa sheria za barabarani na kupunguza ajali zinazohatarisha maisha ya wananchi.

Operesheni hizo zinazotekelezwa kwa ushirikiano na Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA), zimejumuisha ukaguzi wa magari ya uchukuzi wa umma (PSV), waendesha bodaboda pamoja na kutoa elimu kwa abiria na watembea kwa miguu.

Katika Kaunti ya Kilifi, maafisa wa trafiki kutoka kituo cha Rabai kwa ushirikiano na maafisa wa NTSA wameendesha msako wa usiku kando ya barabara kuu ya Mombasa-Nairobi.

Operesheni hiyo imelenga kuondoa barabarani magari yasiyokidhi viwango vya usalama, pamoja na kuhakikisha magari ya uchukuzi wa umma yanafuata masharti yanayotakiwa kisheria kabla ya kuruhusiwa kusafirisha abiria.

Katika Kaunti ya Makueni, maafisa wa trafiki kutoka kituo kidogo cha Kathonzweni wamekutana na waendesha bodaboda pamoja na watembea kwa miguu katika mji wa Kathonzweni, ambapo wamepewa mafunzo kuhusu usalama barabarani.

Waendesha bodaboda wametakiwa kuhakikisha wanafanya upya leseni na nyaraka zao kwa wakati, kuvaa kofia ngumu na makoti yenye vimulimuli, kuzingatia viwango vya mwendo kasi na kujiunga na vyama vya ushirika vya SACCO ili kurahisisha usimamizi wa shughuli zao.

Aidha, wamekumbushwa wajibu wao wa kisheria wa kusimama wanapokutana na ajali na kutoa taarifa kwa polisi badala ya kuendelea na safari kana kwamba hakuna kilichotokea.

Nchini Garissa, maafisa wa trafiki katika kituo cha Premier Bank kando ya barabara ya Kismayu wamewaelimisha waendesha bodaboda kuhusu umuhimu wa kuvaa vifaa vya kujikinga, kuheshimu alama za barabarani na kuzingatia mwendo kasi unaoruhusiwa maeneo ya mijini.

Pia wameonywa dhidi ya kubeba abiria wengi kupita kiwango kinachoruhusiwa, hali inayoweza kuongeza hatari ya ajali.

Katika Kaunti ya Machakos, maafisa wa kituo cha trafiki cha KBC wamefika eneo la Joska kando ya barabara ya Nairobi-Kangundo, ambako wamezungumza na abiria wanaotumia magari ya uchukuzi wa umma.

Abiria wamehimizwa kufunga mikanda ya usalama wakati wote wa safari, kuzingatia nidhamu wanapopanda na kushuka kwenye magari na kuripoti madereva wanaoendesha kwa uzembe.

NPS imesema itaendelea kuimarisha misako na kampeni za uhamasishaji kote nchini, huku ikiwataka madereva, waendesha bodaboda na watembea kwa miguu kuzingatia Sheria za Trafiki ili kuzuia ajali na kuokoa maisha.