Papa Leo XIV amekumbana na tukio lisilo la kawaida wakati wa ziara yake nchini Peru baada ya kitu kilichoaminika kuwa rozari kurushwa kutoka kwa umati na kumpiga karibu na jicho alipokuwa akisalimia waumini akiwa ndani ya gari lake maalumu la wazi.
Tukio hilo lilitokea Jumatatu, Novemba 16, 2026, wakati kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki alipowasili katika kituo cha anga cha Las Palmas jijini Lima kwa ajili ya misa ya kuaga kabla ya kuhitimisha ziara yake nchini humo na kurejea Roma.
Picha na video zilizonaswa wakati wa tukio hilo zilimuonyesha Papa Leo akijaribu kukwepa kitu hicho, lakini kikampiga karibu na jicho, hali iliyomfanya kuligusa na kulisugua eneo hilo muda mfupi baada ya tukio.
Ingawa hakufanikiwa kukidaka kitu hicho, Papa aliendelea kuwasalimia waumini waliokuwa wamekusanyika kando ya njia aliyokuwa akipita kuelekea eneo la misa.
Hakukuwa na dalili zozote kwamba alikuwa amejeruhiwa, huku ratiba yake ikiendelea kama ilivyopangwa.
Tukio hilo limekatiza rekodi yake ya kufanikiwa kudaka vitu mbalimbali ambavyo waumini wamekuwa wakimrushia wakati wa ziara zake za hadhara.
Papa huyo mwenye umri wa miaka 71 amekuwa akivutia watu kutokana na uwezo wake wa kudaka vitu vinavyorushwa kutoka kwa umati, vikiwemo midoli, bendera na zawadi nyingine.
Katika tukio jingine lililovutia watu, aliwahi kusimama na kupokea pizza aliyopewa na wakazi wa Chicago nchini Marekani wakati wa mkutano wa hadhara katika uwanja wa Mtakatifu Petro jijini Roma.
Hata hivyo, si mara ya kwanza kwa jaribio lake la kudaka kitu kutoka kwa umati kuishia bila mafanikio. Katika tukio la awali jijini Roma, Papa aliomba radhi kwa mpiga picha wa Vatican aliyekuwa nyuma ya gari lake baada ya kumgonga alipokuwa akijaribu kudaka kitu kilichokuwa kimetupwa kwake.
Papa Leo alikuwa akihitimisha ziara ya siku 12 katika Amerika Kusini iliyohusisha nchi za Uruguay, Argentina na Peru, huku ziara yake nchini Peru ikidumu kwa siku sita.
Katika hotuba yake wakati wa misa ya kuaga, aliwashukuru wananchi wa Peru kwa mapokezi mazuri na ukarimu waliomwonyesha wakati wa ziara yake, akielezea nchi hiyo kuwa nyumbani kwake.
Papa huyo ana uhusiano wa karibu na Peru ambako aliwahi kuhudumu kama mmisionari na askofu kwa miaka kadhaa kabla ya kuchaguliwa kuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki.
Licha ya tukio hilo, aliendelea na shughuli zake bila kuonyesha dalili za kuathirika, huku safari yake ya kurejea Roma ikiendelea baada ya kumalizika kwa ziara hiyo ya Amerika Kusini.









