Mwanariadha chipukizi wa Kenya, Caren Chepchirchir, ameendeleza makali yake katika riadha ya kimataifa baada ya kutwaa ushindi katika mbio za nyika za Sparkassen Cross Pforzheim nchini Ujerumani, huku Egide Ntakarutimana wa Burundi akishinda upande wa wanaume katika mashindano hayo yaliyofanyika Jumamosi, Novemba 14, 2026.
Chepchirchir mwenye umri wa miaka 17 alionyesha uwezo mkubwa wa kumalizia mbio baada ya kumshinda Francine Niyomukunzi wa Burundi kwa sekunde mbili katika mashindano ya kilomita 7.5 yaliyokuwa yakijumuisha wanariadha wa kitengo cha U23 na wakubwa.
Mkenya huyo alivuka mstari wa mwisho kwa dakika 22:50, huku Niyomukunzi akimaliza kwa dakika 22:52.
Elvanie Nimbona wa Italia alishika nafasi ya tatu kwa dakika 23:19, huku bingwa mtetezi Elena Burkard wa Ujerumani akimaliza wa nne kwa dakika 23:27.
Ushindi huo ni hatua muhimu kwa Chepchirchir katika safari yake ya riadha, hasa ikizingatiwa kuwa ilikuwa mara yake ya kwanza kushiriki mashindano makubwa ya nyika.
Mwanariadha huyo anayejikita zaidi katika mbio za kati za uwanjani, alijipatia medali ya shaba katika mbio za mita 1,500 kwenye Mashindano ya Dunia ya Riadha kwa wanariadha walio chini ya umri wa miaka 20 yaliyofanyika Oregon, Marekani, mwezi Agosti.
Katika upande wa wanaume, Ntakarutimana alishinda mbio hizo kwa namna ya kusisimua baada ya kumzidi Mburundi mwenzake Célestin Ndikumana katika hatua za mwisho.
Wawili hao walimaliza kwa muda sawa wa dakika 19:14, lakini Ntakarutimana akavuka mstari wa mwisho mbele ya Ndikumana baada ya tukio la kushangaza katika mzunguko wa mwisho.
Wanariadha hao walikuwa wamejitenga na wapinzani wao kabla ya kuelekea sehemu ya mwisho ya mashindano, lakini walikosea njia na kuendelea kana kwamba walikuwa wakianza mzunguko mwingine.
Baada ya kuitwa kurejea kwenye mstari wa mwisho, wawili hao walikabiliana katika mbio za mwisho za kasi, Ntakarutimana akitumia uzoefu wake kuhakikisha ushindi.
Rory Leonard wa Uingereza alimaliza wa tatu kwa dakika 19:30, huku Nick Jäger wa Ujerumani akishika nafasi ya nne kwa dakika 19:34.
Mashindano hayo yalikuwa ya kihistoria kwa Pforzheim, yakifanyika kwa mara ya kwanza katika kiwango cha Gold kwenye World Athletics Cross Country Tour.
Kwa Ntakarutimana, ushindi huo ni wa tatu katika mashindano ya Gold ya msimu huu baada ya mafanikio yake Lidingö na Amorebieta-Etxano.
Chepchirchir naye anaendelea kujitengenezea jina katika riadha ya kimataifa, huku ushindi huo ukiongeza matumaini ya Kenya kupata nyota mpya katika mbio za masafa ya kati na nyika.









