Dunia imepata mwezi mwingine wa muda unaozunguka karibu na sayari yetu, ingawa hautadumu kwa muda mrefu angani, huku wanaastronomia wakisema jiwe hilo dogo la angani linatarajiwa kuondoka ndani ya miezi miwili ijayo.
Jiwe hilo, linalojulikana kwa jina la 2026 QQ8, lilitambuliwa kwa mara ya kwanza mwezi Agosti na mwanaastronomia wa Hungary, Krisztián Sárneczky, kabla ya Umoja wa Kimataifa wa Wanaastronomia (IAU) kuthibitisha rasmi uwepo wake mwezi uliopita.
Kwa mujibu wa wataalamu, QQ8 ni miongoni mwa mawe ya angani yanayoweza kuvutwa na nguvu ya dunia na kuzunguka karibu na sayari hiyo kwa kipindi fulani kabla ya kuendelea na safari yake katika anga za mbali.
Jiwe hilo lina ukubwa mdogo sana, likiwa na kipenyo kinachokadiriwa kuwa kati ya mita moja na mbili, huku likiwa umbali wa zaidi ya kilomita 500,000 kutoka Dunia.
Umbali huo ni mkubwa zaidi ya ule uliopo kati ya Dunia na Mwezi wetu wa kawaida, ambao uko takribani kilomita 384,400 kutoka sayari yetu.
Hata hivyo, tofauti na Mwezi wa kawaida ambao umekuwa ukizunguka Dunia kwa mabilioni ya miaka, miezi ya muda huwa ni wageni wa angani wanaokaa karibu na sayari yetu kwa muda mfupi kutokana na mabadiliko ya nguvu za uvutano.
Wanaastronomia wanaamini kuwa Dunia huenda iligusana na jiwe hilo la angani mwaka 2026, huku tukio la mtikisiko lililorekodiwa mwezi Aprili likitajwa kuwa mojawapo ya viashiria vinavyoweza kuhusishwa na tukio hilo.
Ingawa uwepo wa QQ8 umeibua shauku miongoni mwa wataalamu wa anga, maisha yake karibu na Dunia yanaelekea kufikia mwisho hivi karibuni.
Wataalamu wanatarajia jiwe hilo kuondoka katika eneo la uvutano wa Dunia ndani ya miezi miwili ijayo na kurejea katika safari yake ya kawaida angani.
Ugunduzi wa miezi hiyo ya muda huwapa wanaastronomia fursa ya kuchunguza jinsi mawe ya angani yanavyoingiliana na sayari ya dinia, pamoja na kuelewa zaidi kuhusu nguvu za mvutano zinazotawala mfumo wa jua.
Pamoja na ukubwa wake mdogo, QQ8 inaongeza ushahidi kuwa Dunia inaweza kuwa na wageni wa muda angani ambao hawajulikani kwa urahisi, lakini wanaoweza kutoa taarifa muhimu kuhusu historia na mienendo ya mfumo wetu wa jua.









