Mwanamke mwenye umri wa miaka 23 amefikishwa katika mahakama ya Eldoret kufuatia tuhuma za kumuua mwanawe mchanga kwa kumnyonga hadi kufariki, wiki mbili pekee baada ya kujifungua, katika kisa kinachodaiwa kuchochewa na mzozo wa malezi baada ya mpenzi wake kukataa kuwajibika kumlea mtoto huyo.
Mshukiwa huyo, Sharon Chepkurui, ambaye anafanya kazi kama mlinzi katika shule moja ya kibinafsi, hata hivyo, hakufunguliwa mashtaka baada ya afisa wa polisi anayechunguza kesi hiyo kuomba muda zaidi wa kukamilisha uchunguzi.
Afisa wa upelelezi, Dorothy Matete, aliomba mahakama kumpa siku 14 ili kukamilisha uchunguzi na kukusanya ushahidi zaidi kuhusiana na mazingira ya kifo cha mtoto huyo.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyowasilishwa mahakamani, Chepkurui anadaiwa kujifungia ndani ya nyumba yake baada ya kurejea kutoka hospitalini alipokuwa amejifungua mtoto wa kiume.
Inadaiwa kuwa baada ya mpenzi wake kukataa kushiriki katika majukumu ya malezi ya mtoto huyo, mshukiwa aliamua kumuua kwa kumnyonga kabla ya kuuweka mwili wake ndani ya mfuko na kuuficha katika chumba chake cha kulala.
Tukio hilo lilianza kufichuka baada ya Chepkurui kurejea kazini, ambapo wafanyakazi wenzake walimuuliza kuhusu mtoto wake mchanga lakini akashindwa kutoa maelezo ya kuridhisha kuhusu alikokuwa.
Wafanyakazi hao walizidi kuwa na wasiwasi kutokana na kutopatikana kwa mtoto huyo na hatimaye kutoa taarifa kwa maafisa wa polisi katika kituo cha Ainaptich, eneo bunge dogo la Moiben, Kaunti ya Uasin Gishu.
Baada ya kupokea taarifa hizo, maafisa wa polisi walianzisha msako uliowafikisha katika makazi ya mshukiwa, ambako walifanya upekuzi na kugundua mwili wa mtoto huyo katika eneo ambalo anadaiwa kuuficha.
Chepkurui alikamatwa na kuwasilishwa mbele ya mahakama ya Eldoret ili hatua zaidi za kisheria zichukuliwe huku uchunguzi ukiendelea kubaini kwa kina kilichosababisha kifo cha mtoto huyo.
Hakimu mkuu wa mahakama ya Eldoret, Peter Ndwiga, alikubali ombi la upande wa mashtaka na kuamuru mshukiwa azuiliwe katika kituo cha polisi cha Central jijini Eldoret kwa siku 14.
Mahakama ilielekeza kuwa mshukiwa huyo azuiliwe hadi Novemba 23, 2026, ambapo kesi hiyo itatajwa tena ili kufahamu maendeleo ya uchunguzi na hatua zitakazofuata.
Polisi wanatarajiwa kukamilisha uchunguzi kabla ya tarehe hiyo ili kubaini iwapo kuna ushahidi wa kutosha kumfungulia Chepkurui mashtaka rasmi kuhusiana na kifo cha mwanawe.
Kisa hicho kimeibua maswali kuhusu usalama wa watoto wachanga na wajibu wa wazazi katika malezi, huku uchunguzi ukiendelea kubaini mazingira kamili ya mkasa huo.









