Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ameondolewa katika shtaka la uhaini lililokuwa likimkabili baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.
Mahama imesema kuwa kosa hilo halijathibitishwa, hata hivyo amepatikana na hatia ya kosa dogo la uchochezi.
Katika hukumu iliyotolewa Ijumaa, Novemba 6, 2026, Mahakama imemuondolea Lissu shtaka la uhaini ambalo lilikuwa likimuweka hatarini kukabiliwa na adhabu ya kifo endapo angepatikana na hatia.
Uamuzi huo umetolewa baada ya jopo la majaji watatu kutathmini ushahidi uliowasilishwa na upande wa Jamhuri pamoja na mawasilisho ya upande wa utetezi katika kesi hiyo iliyodumu kwa takribani mwaka mmoja.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa kuhusu hukumu hiyo, upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kwamba Lissu alikuwa na nia ya kutenda kosa la uhaini kwa kuchochea wananchi kuvuruga Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa madhumuni ya kuitishia Serikali.
Hata hivyo, Mahakama imempata na hatia ya kosa dogo la uchochezi, hatua inayomaanisha kuwa kuondolewa kwa shtaka la uhaini hakumaanishi kuwa ameachiwa huru katika mashtaka yote yaliyokuwa yakijadiliwa.
Lissu alikuwa akikabiliwa na shtaka la uhaini chini ya kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, kufuatia matamshi aliyodaiwa kutoa Aprili 3, 2025, katika makao makuu ya Chadema jijini Dar es Salaam.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa katika mkutano huo, Lissu alitoa matamshi yaliyolenga kuwahamasisha wananchi kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kuchochea uasi na kuvuruga mchakato wa uchaguzi.
Hata hivyo, Lissu alikanusha kutenda kosa la uhaini, akisisitiza kuwa matamshi yake hayakufikia kiwango cha kisheria kinachohitajika kuthibitisha shtaka hilo.
Kesi hiyo ilisikilizwa na jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Uamuzi huo ni miongoni mwa matukio makubwa katika historia ya kesi za kisiasa nchini Tanzania, kutokana na uzito wa shtaka lililokuwa likimkabili Lissu na adhabu iliyokuwa ikihusishwa nalo.
Hukumu hiyo sasa inafungua ukurasa mwingine katika safari ya kisiasa na kisheria ya mwenyekiti huyo wa Chadema, huku suala la hatia ya uchochezi likibaki kuwa sehemu muhimu ya matokeo ya kesi hiyo.









