Binti wa aliyekuwa mtangazaji wa televisheni nchini Kenya, Regina Re, amekana mashtaka ya kumuua nyanya yake mwenye umri wa miaka 86, katika kesi iliyozua mjadala mkubwa kufuatia mazingira ya kutatanisha ya kifo cha mwanamke huyo jijini Nairobi.
Thandie Malaika Wanjiku Gitao amekana kumuua Dorita Lasinder Macharia, huku mahakama ikiagiza afanyiwe uchunguzi wa afya ya akili katika Hospitali ya Kaunti ya Kiambu Level 5 ili kubaini hali yake ya kiakili na iwapo anafaa kuendelea na mchakato wa kesi hiyo.
Kesi hiyo inahusiana na tukio la Oktoba 30, 2026, ambapo Dorita alipatikana akiwa amefariki ndani ya nyumba yake katika eneo la Loresho Ridge, Nairobi, akiwa na majeraha makubwa yaliyotokana na kitu chenye makali.
Uchunguzi wa mwili uliofanywa Novemba 3 na daktari wa serikali, Dkt. Bernard Midia, ulibaini kuwa marehemu alifariki kutokana na kupoteza damu nyingi baada ya kupata majeraha kadhaa, yakiwemo majeraha mawili ya kuchomwa shingoni yaliyoharibu mishipa mikubwa ya damu.
Kabla ya kifo chake, uchunguzi wa polisi uliwasilisha madai kuwa Dorita alikuwa ameingia katika mzozo na mjukuu wake baada ya kudaiwa kumkuta akiwa katika hali isiyofaa na mpenzi wake ndani ya nyumba.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyowasilishwa mahakamani na afisa wa upelelezi, marehemu alimtaka Thandie kuondoka nyumbani kwake na kurejesha funguo za chumba alichokuwa akitumia.
Inadaiwa kuwa baada ya mabishano hayo, Thandie aliondoka lakini baadaye akarudi na kukaa ndani ya nyumba hiyo na nyanya yake kwa takribani saa moja kabla ya mwanamke huyo kupatikana akiwa amejeruhiwa vibaya.
Kesi hiyo pia imehusisha mama yake Thandie, Regina Wambui Macharia Gitao, maarufu kama Regina Re, pamoja na ndugu yake Alton Jimmy Macharia.
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Renson Ingonga, aliidhinisha mashtaka tofauti dhidi ya watatu hao, ambapo Thandie anakabiliwa na shtaka la mauaji huku Regina na Alton wakituhumiwa kusaidia kuficha ushahidi baada ya tukio hilo.
Hata hivyo, madai dhidi yao bado yanahitaji kuthibitishwa mahakamani.
Mpenzi wa Thandie, Immanuel Munyeki, ambaye awali alikuwa miongoni mwa washukiwa, aliachiliwa Novemba 12 baada ya wachunguzi kusema hawakupata ushahidi unaomhusisha na mauaji hayo.
Kesi hiyo imevutia hisia za umma kutokana na kuhusisha familia moja na madai mazito ya mauaji ya mama mwenye umri mkubwa, huku hatua inayofuata ya mahakama ikitarajiwa kutegemea matokeo ya uchunguzi wa afya ya akili wa Thandie.









