Safari ya mwanabasketball kutoka Marekani kwenda Nigeria kwa madai ya kutafuta fursa za kukuza taaluma yake imegeuka kuwa kisa cha kukamatwa na maafisa wa kupambana na dawa za kulevya baada ya kukutwa na shehena ya bangi yenye uzito wa karibu kilo 34 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Murtala Muhammed jijini Lagos.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28, Greene Da’monte Khiree, alikamatwa Novemba 11, 2026, baada ya kuwasili nchini Nigeria akitokea Thailand kupitia Dubai kwa ndege ya shirika la Emirates.
Kwa mujibu wa Shirika la Kupambana na Dawa za Kulevya Nigeria (NDLEA), Khiree alikuwa akisafiri na mabegi mawili yaliyokuwa yamehifadhiwa kwenye sehemu ya mizigo ya ndege, lakini alitiliwa shaka baada ya kuyaacha mabegi hayo na kujaribu kuondoka uwanja wa ndege akiwa na mzigo wake wa mkononi pekee.
Maafisa waliokuwa wakimfuatilia kwa siri walimkamata katika maegesho ya magari ya uwanja huo kabla ya kuyafanyia ukaguzi mabegi aliyoyaacha.
Ukaguzi huo ulifichua vifurushi 32 vya bangi aina ya Loud, ikiwa na uzito wa jumla wa kilo 33.95. Kila begi lilikuwa na vifurushi 16, huku kifaa cha kufuatilia mahali kilipo mzigo kikidaiwa pia kupatikana ndani ya mabegi hayo.
Khiree, ambaye anatoka Savannah, jimbo la Georgia nchini Marekani, aliwaambia wachunguzi kuwa amekuwa akiishi Thailand tangu Oktoba 2025 ambako amekuwa akicheza mchezo wa kikapu katika ngazi ya kulipwa.
Alidai kuwa safari yake ya Nigeria ilikuwa ya mapumziko pamoja na kutafuta watu na mitandao mipya ambayo ingemsaidia kupanua fursa za taaluma yake ya kikapu.
Hata hivyo, maelezo yake hayakuonekana kumaliza maswali ya wachunguzi baada ya uchunguzi wa kitaalamu wa simu yake ya mkononi kudaiwa kubaini taarifa zilizomhusisha na shughuli za usafirishaji wa dawa hizo za kulevya.
Kwa mujibu wa taarifa za NDLEA, uchunguzi wa simu hiyo ulionyesha kuwa huenda alikuwa na ufahamu kuhusu mzigo huo na kuhusika katika operesheni ya kuusafirisha.
Kisa cha Khiree ni sehemu ya operesheni kubwa ya NDLEA dhidi ya mitandao ya biashara haramu ya dawa za kulevya nchini Nigeria.
Katika tukio jingine kwenye uwanja huo huo, maafisa walikamata mwanamume mwenye umri wa miaka 56 aliyekuwa na kilo 25.05 za methamphetamine zilizofichwa ndani ya vifurushi vya nafaka za kiamsha kinywa vilivyoagizwa kutoka Afrika Kusini.









