Serikali ya Israel imepanua mpango wa kuwashawishi raia wa mataifa ya Afrika wanaoishi nchini humo kuondoka kwa hiari, ikiwemo Wakenya na Watanzania, kwa kuwapa Dola 3,500 (takribani Sh455,000) pamoja na tiketi ya ndege ya bure.
Hatua hiyo imeongeza wigo wa watu wanaoweza kunufaika na mpango huo, ambao awali ulikuwa ukihusisha raia wa mataifa machache ya Afrika, yakiwemo Eritrea, Sudan na Ethiopia.
Kwa mujibu wa taarifa kuhusu mabadiliko hayo, mpango huo mpya ulianza kutekelezwa Novemba 9, 2026, na unatarajiwa kuendelea hadi Desemba 31 mwaka huu.
Hata hivyo, si kila raia wa Afrika anayeishi Israel anastahili kupata fedha hizo, kwani mpango huo una masharti maalumu yanayopaswa kutimizwa kabla ya kuidhinishwa.
Miongoni mwa wanaostahili ni raia wa mataifa ya Afrika ambao wameishi Israel kwa zaidi ya miaka miwili bila kuwa na vibali halali vya uhamiaji, pamoja na baadhi ya wenye vibali vya muda vya kuishi nchini humo.
Pia, mpango huo unawahusisha watu walioingia Israel kihalali lakini wakabaki nchini humo baada ya muda wa viza zao kuisha.
Waombaji wanatakiwa kuwasilisha maombi yao kupitia mtandao au kufika katika ofisi za Mamlaka ya Idadi ya Watu na Uhamiaji nchini Israel, ambako watafanyiwa mahojiano ili kuthibitisha kuwa wameamua kuondoka kwa hiari.
Baada ya kukamilisha taratibu hizo na kupata nyaraka zinazohitajika za kusafiria, mamlaka husika itaratibu safari zao na kugharamia tiketi za ndege.
Fedha hizo zitatolewa taslimu katika uwanja wa ndege kabla ya abiria kupanda ndege kuelekea wanakokwenda.
Aidha, waombaji watakaokubaliwa wanaweza kupata ulinzi dhidi ya kukamatwa kwa hadi wiki mbili kabla ya siku yao ya kuondoka, ili kuwawezesha kukamilisha maandalizi ya safari.
Uamuzi huo unajiri huku idadi ya wahamiaji wa Afrika wanaoondoka Israel kwa msaada wa serikali ikiripotiwa kupungua kwa takribani asilimia 20.
Takwimu zinaonyesha kuwa watu 3,511 waliondoka nchini humo kupitia mpango huo mwaka 2024, lakini idadi hiyo ikashuka hadi 2,815 mwaka 2025.
Mamlaka za Israel zimehusisha kupungua kwa idadi hiyo na kupungua kwa nafasi za kuhamia nchi nyingine kama Canada, udhibiti mkali wa mipaka nchini Marekani pamoja na changamoto za usafiri wa anga zilizochangiwa na migogoro ya kikanda.
Kwa kupanua mpango huo kwa mataifa yote ya Afrika, Israel inalenga kuongeza idadi ya wageni wanaokubali kuondoka nchini humo bila kulazimishwa kupitia taratibu za kuwafurusha.









