Mahakama Kuu imekataa kuidhinisha kama ya dharura kesi inayotaka Serikali kueleza jinsi Sh17.5 bilioni zilizotengwa kwa mradi wa maji chini ya ardhi katika kaunti tano kame zilivyotumika.
Katika uamuzi uliotolewa Oktoba 29, 2026, Jaji Patricia M. Nyaundi alisema ombi lililowasilishwa na Francis Awino Oktoba 27 halijakidhi vigezo vya kuthibitishwa kuwa la dharura.
Hata hivyo, mahakama imeelekeza kuwa ombi hilo liwasilishwe rasmi kwa washitakiwa na wahusika wengine kabla ya Novemba 5, 2026, huku wakipewa siku 14 kuwasilisha majibu yao au kufikia Novemba 20.
Awino ataruhusiwa kuwasilisha affidavit ya ziada ndani ya siku saba baada ya kupokea majibu hayo.
Kesi hiyo itatajwa tena Februari 10, 2027 kwa ajili ya kuthibitisha uzingatiaji wa maagizo ya mahakama na kutoa maelekezo zaidi.
Ombi hilo linahusu Horn of Africa Groundwater for Resilience Project, mradi mkubwa wa maendeleo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia mkopo wa takriban dola milioni 135 za Marekani, sawa na Sh17.5 bilioni.
Mradi huo unalenga kuimarisha upatikanaji wa maji chini ya ardhi na kuongeza uwezo wa jamii kukabiliana na ukame katika kaunti za Turkana, Marsabit, Mandera, Wajir na Garissa.
Katika kesi hiyo, Awino anataka mahakama itoe amri za kulinda nyaraka zote za mradi, zikiwemo rekodi za kifedha, zabuni, mikataba, stakabadhi za malipo, taarifa za benki, ripoti za utekelezaji na kumbukumbu za visima vya maji na ufuatiliaji.
Pia anataka wahusika wazuiwe kuharibu, kuficha, kubadilisha au kufuta nyaraka hizo, iwe katika mfumo wa kielektroniki au wa kawaida.
Zaidi ya hayo, anataka Mamlaka ya Rasilimali za Maji (WRA) na Waziri wa Maji kuwasilisha ripoti ya awali iliyothibitishwa ndani ya siku 14, ikionyesha fedha zote zilizoidhinishwa, kupokelewa na kutumika, mikataba iliyotolewa na malipo yaliyofanywa.
Ripoti hiyo pia inapaswa kueleza hali ya utekelezaji wa visima vya uchunguzi na ufuatiliaji pamoja na kazi zilizokamilika na zinazobaki katika kila kaunti.
Awino pia anataka ufafanuzi kuhusu nafasi rasmi na ushiriki wa Mohammed Shurie katika usimamizi na uendeshaji wa mradi huo.
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) wameorodheshwa kama wahusika wengine katika kesi hiyo.
Katika misingi ya ombi lake, Awino anasema kesi hiyo inazua maswali muhimu ya kikatiba kuhusu uwazi, uwajibikaji na matumizi bora ya fedha za umma.
Anasisitiza kuwa madai yake hayajengi hitimisho kwamba fedha zimeibwa, bali yanatokana na haja ya kupata taarifa zinazoweza kuthibitishwa kuhusu namna fedha zilivyopokelewa, kutolewa kwa mikataba na kugeuzwa kuwa miradi halisi ya maji.
Anarejelea ripoti ya ujumbe wa Benki ya Dunia wa Machi 10 hadi 14, 2025, pamoja na taarifa ya utekelezaji ya Wizara ya Maji ya Novemba 26, 2025, akisema nyaraka hizo zinaonyesha umuhimu wa kupata maelezo ya kina kuhusu matumizi ya fedha na utekelezaji wa mradi.
Awino anasema amri anazoomba hazitalenga kusimamisha mradi wala huduma muhimu za maji, bali kuhakikisha kuwa fedha, mikataba na malipo vinaendeshwa kwa mujibu wa Katiba huku rekodi muhimu zikilindwa.









