Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, ameibua mjadala mpya kuhusu usawa katika ugawaji wa nafasi za uongozi serikalini baada ya kuitumia kauli mbiu ya Rais William Ruto, ‘Usawa ni Sawa’, kuzungumzia uteuzi wa viongozi wapya katika taasisi za umma.

Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X kupitia akaunti yake ya @rigathi, Gachagua alichapisha picha ya taarifa rasmi ya Tume ya Huduma za Walimu (TSC) iliyotangaza kuteuliwa kwa Cheptumo Ayabei kuwa Katibu na Afisa Mkuu Mtendaji mpya wa tume hiyo, kisha kuandika kwa ufupi, “Usawa Ni Sawa"

Ujumbe huo unaonekana kuwa kejeli dhidi ya kauli inayotumiwa mara kwa mara na Rais Ruto kuelezea msimamo wa serikali yake kuhusu usawa na kuhakikisha maeneo yote nchini yananufaika na fursa za maendeleo.

Kauli hiyo inajiri wakati serikali ya Ruto imetangaza pia uteuzi wa Lydia Sitienei Chelagat kuwa mteule wa nafasi ya Kamishna wa Ulinzi wa Data (Data Commissioner), akichukua nafasi ya Immaculate Kassait ambaye muda wake wa kuhudumu unatarajiwa kumalizika.

Chelagat, ambaye amewahi kuhudumu kama Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria katika Mamlaka ya Mawasiliano nchini Kenya (CA), amependekezwa na Rais Ruto na jina lake kuwasilishwa katika Bunge la Kitaifa kwa ajili ya kuidhinishwa kabla ya kushika wadhifa huo.

Nafasi hiyo inahusika na kusimamia utekelezaji wa sheria za ulinzi wa taarifa binafsi nchini, wakati matumizi ya huduma za kidijitali yakizidi kupanuka katika sekta za umma na binafsi.

Gachagua amekuwa akiikosoa serikali ya Ruto kuhusu kile anachodai kuwa ukosefu wa uwiano katika ugawaji wa nafasi za ajira na uteuzi wa viongozi katika taasisi za umma.

Kiongozi huyo wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) amekuwa akisisitiza kuwa usawa unapaswa kuonekana katika vitendo, hususan katika ajira za serikali, uteuzi wa viongozi na ugawaji wa miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake, Rais Ruto amekuwa akitetea kauli mbiu ya ‘Usawa ni Sawa’ akisema serikali yake inalenga kuhakikisha hakuna jamii wala eneo linaloachwa nyuma katika ajenda ya maendeleo ya nchi.

Ujumbe wa Gachagua unaendeleza mvutano wa kisiasa kati yake na aliyekuwa mkuu wake, huku suala la uwakilishi wa jamii mbalimbali katika nafasi za kitaifa likiendelea kuwa sehemu ya mijadala ya kisiasa nchini Kenya.