Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Miami nchini Marekani ulilazimika kusimamisha kwa muda safari za ndege zilizokuwa zikielekea katika uwanja huo baada ya ndege ya mizigo ya kampuni ya FedEx kupita mwisho wa njia ya kutua (runway) Jumatano usiku, Novemba 25, 2026.
Tukio hilo lilisababisha shughuli za usafiri wa anga kuvurugika katika uwanja huo, huku mamlaka zikifunga kwa muda njia zote za kutua na kuruka ndege isipokuwa moja ili kuruhusu shughuli za dharura na uchunguzi kufanyika.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Marekani (FAA), ndege hiyo aina ya McDonnell Douglas MD-11 ilikuwa imewasili kutoka Memphis ilipopata tatizo wakati wa kutua na kupita nje ya njia iliyotengwa.
Tukio hilo liliripotiwa kutokea majira ya saa 2:40 usiku kwa saa za Miami, huku vikosi vya zimamoto na uokoaji vya Miami-Dade vikifika eneo la tukio kushughulikia hali hiyo.
Hakuna mtu aliyeripotiwa kujeruhiwa katika tukio hilo, huku kampuni ya FedEx ikithibitisha kuwa wafanyakazi wote waliokuwa ndani ya ndege hiyo walikuwa salama.
Katika taarifa yake, kampuni hiyo ilisema ndege hiyo ilikumbwa na tatizo wakati wa kutua na kwamba inaendelea kushirikiana na mamlaka zinazochunguza chanzo cha tukio hilo.
Kusimamishwa kwa safari hizo kulisababisha ucheleweshaji wa ndege zilizokuwa zikielekea Miami, huku baadhi ya safari zikikabiliwa na kuchelewa kwa takribani saa moja.
FAA ilitarajia safari kurejea katika hali ya kawaida baada ya muda mfupi, huku uwanja huo ukiwataka abiria kuwasiliana na mashirika yao ya ndege kupata taarifa kuhusu ratiba zilizobadilika.
Tukio hilo limetokea siku moja kabla ya sikukuu ya Thanksgiving nchini Marekani, kipindi ambacho huwa na ongezeko kubwa la wasafiri wanaosafiri kwenda maeneo mbalimbali nchini humo.
Hata hivyo, tukio hilo limeibua kumbukumbu za ajali nyingine iliyohusisha ndege ya mizigo ya Amazon katika uwanja huo mwezi Septemba mwaka huu, ambapo ndege hiyo ilipita nje ya njia ya kutua na kusababisha vifo vya watu watano waliokuwa ardhini.
Ingawa ndege ya FedEx ilitua kwenye runway tofauti na ile iliyohusika katika tukio la Amazon, njia kadhaa za kutua katika uwanja huo hukutana upande wa magharibi, hali iliyosababisha ndege hiyo kuishia karibu na eneo lililohusishwa na ajali ya awali.
Aidha, ndege aina ya MD-11 imekuwa chini ya uangalizi wa mamlaka za usafiri wa anga kufuatia ajali iliyohusisha ndege ya UPS nchini Kentucky mwaka jana, ambapo watu 15 walifariki baada ya injini ya ndege kuanguka wakati wa kuruka.
FAA imesema itachunguza tukio la Miami kubaini kilichosababisha ndege hiyo kupita mwisho wa njia ya kutua.









