Katibu Mkuu katika Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari anayesimamia Utangazaji na Mawasiliano, Stephen Isaboke, amewataka wahariri wa vyombo vya habari nchini kutumia busara na weledi wanaporipoti kauli za wanasiasa zinazochochea chuki za kikabila, uhasama na vitisho vya ghasia dhidi ya jamii mbalimbali.

Isaboke amesema vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kulinda umoja wa kitaifa kupitia namna vinavyoripoti mijadala ya kisiasa, hasa wakati huu ambapo Kenya inaelekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa Kongamano la Tisa la Mwaka la Wahariri nchini lililoandaliwa na Chama cha Wahariri Kenya (Kenya Editors' Guild) mjini Mombasa, Isaboke amesisitiza kuwa kuna tofauti kubwa kati ya kuripoti matamshi ya uchochezi kwa maslahi ya umma na kuyapa nafasi ya kusambaa zaidi kupitia vyombo vya habari.

Amesema waandishi wa habari na wahariri wanapaswa kutambua kuwa jukumu lao si kurudia kila kauli inayotolewa na wanasiasa bila kuzingatia athari zake kwa jamii, usalama wa wananchi na mshikamano wa kitaifa.

Kwa mujibu wa Isaboke, ushindani wa kupata vichwa vya habari vinavyovutia wasomaji, kuongeza watazamaji na kuvutia watu kwenye majukwaa ya kidijitali haupaswi kuwa sababu ya vyombo vya habari kuachana na misingi ya taaluma ya uandishi wa habari.

Amesema uadilifu wa kitaaluma na usalama wa wananchi vinapaswa kupewa kipaumbele kuliko maslahi ya kibiashara yanayotokana na idadi ya wasomaji, watazamaji au mibofyo kwenye mitandao.

"Utafutaji wa vichwa vya habari, viwango vya watazamaji na trafiki ya kidijitali haupaswi kamwe kushinda uadilifu wa kitaaluma, usalama wa umma na mshikamano wa kitaifa. Vyombo vyetu vya habari vinapaswa kujilinda dhidi ya kuwa njia ya kusambaza matamshi ya migawanyiko, uhamasishaji wa kikabila na kugawanyika kwa nchi yetu," amesema Isaboke.

Onyo hilo linajiri wakati ambapo shughuli za kisiasa zikianza kushika kasi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, kipindi ambacho kauli za viongozi na wanasiasa kuhusu jamii, makabila na ushindani wa kisiasa zinaweza kuwa na athari kwa utulivu wa nchi.

Isaboke amesisitiza umuhimu wa wahariri kuhakikisha taarifa zinazohusu matamshi yenye utata zinachunguzwa na kuwasilishwa kwa muktadha unaofaa badala ya kuzitumia kama nyenzo za kuongeza umaarufu wa habari.

Amesema vyombo vya habari vina jukumu la kuhabarisha umma kwa uwajibikaji huku vikihakikisha kuwa uhuru wa habari unaambatana na kuzingatia usalama, amani na mshikamano wa Wakenya.

Kongamano hilo la mwaka la wahariri linawakutanisha wadau wa sekta ya habari kujadili masuala yanayohusu taaluma ya uandishi wa habari, changamoto zinazokabili vyombo vya habari na nafasi yake katika kulinda demokrasia nchini.