Chama cha Equitable Party nchini Kenya kimeiomba Mahakama ya Kutatua Migogoro ya Vyama vya Siasa (PPDT) kutupilia mbali kesi inayolenga kuzuia mpango wake wa kubadili jina na kuwa Linda Mwananchi Movement, kikisema mlalamishi hana msingi wa kisheria kupinga uamuzi uliofanywa kabla hajajiunga na chama hicho.

Katika hati ya majibu iliyowasilishwa mbele ya mahakama hiyo jijini Nairobi, Katibu Mkuu wa chama hicho, Italima Motanya, amepinga ombi lililowasilishwa na Emmanuel Willyngtone Khamala, akidai kuwa alijiunga na chama hicho Oktoba 11, 2026, siku tatu baada ya Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) kuidhinisha mabadiliko ya jina Oktoba 8.

Motanya amesema Khamala hawezi kupinga uamuzi huo kwa kuwa wakati ulipofanywa hakuwa mwanachama wa chama hicho, huku akitilia shaka sababu za kujiunga na chama kisha kuwasilisha malalamiko kuhusu uamuzi uliokuwa tayari umetangazwa.

Aidha, chama hicho kimehoji uanachama wa Khamala kikisema hajawasilisha cheti cha kuthibitisha kuwa ni mwanachama aliyesajiliwa, kama inavyotakiwa chini ya katiba ya chama hicho.

Katika hoja nyingine, Equitable Party imedai kuwa mlalamishi alikiuka utaratibu wa ndani wa kutatua migogoro kabla ya kuwasilisha kesi katika mahakama hiyo, kinyume na Kifungu cha 40(2) cha Sheria ya Vyama vya Siasa.

Kwa mujibu wa Motanya, chama kilipokea barua ya malalamiko kutoka kwa Khamala Novemba 6, 2026, na siku iliyofuata kilimjulisha kuwa suala lake limewasilishwa kwa kamati ya ndani ya kutatua migogoro, huku akialikwa kuhudhuria kikao cha kusikilizwa kwa mdomo.

Hata hivyo, amesema mlalamishi hakujibu simu wala ujumbe uliopelekwa kwake kuwezesha mchakato huo kuendelea, badala yake akaamua kuwasilisha kesi katika mahakama hiyo.

Chama hicho pia kimepinga uhalali wa barua inayodaiwa kuandikwa Oktoba 28, kikisema haikuwa na saini na haikupokelewa katika ofisi zake.

Kuhusu mabadiliko ya jina, Motanya amesema Kamati Kuu ya Kitaifa ilifanya kikao chake kwa mujibu wa katiba na kwamba Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (National Delegates Congress) lililofanyika Novemba 13, 2026, lilifuata taratibu zilizowekwa.

Amesisitiza kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa ndiye mwenye mamlaka ya kisheria kuthibitisha mabadiliko ya majina, nembo na katiba za vyama.

Katika kesi hiyo, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna ametajwa kuwa mhusika mwenye maslahi (interested party), huku mlalamishi akitaka kuzuiwa kwa uamuzi wa chama hicho.

Shauri hilo linasikilizwa chini ya nambari PPDTC No. E029 of 2026 kufuatia ombi lililowasilishwa Novemba 16, 2026.