Mahakama Kuu imeizuia Wizara ya Afya kuanza kuendesha kituo kinachohusishwa na udhibiti wa Ebola katika kambi ya kijeshi ya Laikipia Airbase, hadi serikali itakapoweka wazi nyaraka muhimu kuhusu uanzishwaji, usalama na uendeshaji wa mradi huo.

Katika uamuzi wake, mahakama imeipa wizara hiyo siku 45 kuwasilisha mikataba, tathmini za usalama, vibali vya udhibiti na nyaraka za tathmini ya athari za kimazingira zinazohusiana na kituo hicho.

Mahakama imeelekeza serikali kufichua makubaliano na hati za maelewano iliyofanya na washirika wengine waliohusika katika mradi huo, pamoja na tathmini za afya ya umma, usalama wa viumbe na ripoti za kiusalama.

Aidha, wizara inatakiwa kubainisha iwapo ilipata idhini kutoka kwa Bunge, mamlaka za udhibiti pamoja na serikali ya kaunti husika kabla ya kuanzisha kituo hicho.

Mahakama pia imetaka kuwekwa wazi taratibu zitakazotumika kuwapokea, kuwatenga, kuwahudumia na kuwatibu watu wanaoshukiwa kuwa na Ebola au waliokutana na waathiriwa wa ugonjwa huo.

Uamuzi huo umetolewa baada ya kuunganishwa kwa maombi kadhaa ya kikatiba yaliyopinga kuanzishwa kwa kituo hicho, huku waombaji wakieleza wasiwasi kuhusu usalama wa wananchi, uwazi wa serikali na uwezekano wa kukiukwa kwa haki za kimsingi za wakazi wa Laikipia.

Waombaji walikuwa wamehoji kuwa mradi huo unaweza kuathiri haki ya kuishi, kupata huduma za afya, haki ya kupata usikilizwaji wa haki katika maamuzi ya kiutawala na haki ya kupata haki kupitia mahakama.

Katika uamuzi wake, mahakama ilibaini kuwa Wizara ya Afya ilishindwa kutekeleza wajibu wake wa kikatiba wa kutoa taarifa zilizoombwa na waombaji, hatua iliyokiuka Kifungu cha 35(3) cha Katiba ya Kenya.

Jaji pia alisisitiza kuwa ushirikishwaji wa wananchi ni sharti la lazima chini ya Kifungu cha 10 cha Katiba, hasa pale ambapo maamuzi ya serikali yana athari kubwa kwa jamii.

Mahakama ilitilia shaka sababu za serikali kuanzisha kituo cha umuhimu huo katika Kaunti ya Laikipia bila kuwafahamisha wakazi kuhusu madhumuni yake, namna kitakavyoendeshwa na hatua za usalama zitakazowekwa.

Aidha, ilikataa msimamo kwamba wananchi wanapaswa kutegemea tu ahadi za serikali kuhusu usalama wao bila kupewa nyaraka zinazothibitisha kuwa maslahi yao yamezingatiwa.

Hata hivyo, mahakama ilitambua wajibu wa serikali kulinda nchi dhidi ya dharura za kiafya, ikiwemo milipuko ya Ebola, lakini ikasema jukumu hilo haliiondolei serikali wajibu wa kufuata Katiba.

Kutokana na uamuzi huo, Wizara ya Afya imezuiwa kuendelea na ujenzi au kuanza kuendesha kituo hicho hadi itakapowasilisha nyaraka zinazohitajika na mahakama kuthibitisha kuwa imetekeleza maagizo hayo.