Waziri wa Utumishi wa Umma, Geoffrey Ruku, amewapa wakuu wa taasisi za serikali hadi Desemba 20, 2026, kuhakikisha wamejiunga na mfumo wa kidijitali wa usimamizi wa rasilimali watu (HRIS), akionya kuwa watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo watachukuliwa hatua za kinidhamu na kutangazwa hadharani.
Ruku amesema zaidi ya taasisi 200 za serikali bado hazijaunganisha shughuli zao katika mfumo huo, licha ya kuwepo kwa agizo la awali la Baraza la Mawaziri lililotaka taasisi zote za umma kuutekeleza.
Waziri huyo ameonya kuwa serikali itachapisha orodha ya taasisi ambazo zitakuwa hazijatii agizo hilo pamoja na majina ya wakurugenzi wake kabla ya Krismasi, hatua aliyoitaja kama ‘Orodha ya Aibu’.
Amesisitiza kuwa Desemba 20 ni tarehe ya mwisho isiyoweza kuongezwa, akipuuza kile alichokitaja kuwa visingizio vinavyotolewa na baadhi ya viongozi wa taasisi kuchelewesha utekelezaji wa agizo hilo.
Kwa mujibu wa Ruku, mfumo wa HRIS ni sehemu muhimu ya mageuzi yanayolenga kuboresha utendaji wa utumishi wa umma, kudhibiti matumizi ya fedha za serikali na kuondoa wafanyakazi hewa pamoja na malipo ya mishahara yanayojirudia.
Amefichua kuwa uchunguzi wa mifumo ya mishahara umebaini baadhi ya wafanyakazi wamekuwa wakilipwa mishahara na taasisi mbili tofauti za serikali kwa wakati mmoja.
Aidha, ukaguzi wa kiuchunguzi umebaini madai ya baadhi ya mameneja na wasimamizi wa mifumo ya rasilimali watu kutumia vibaya mifumo hiyo kwa kufanya upandishaji vyeo na kuongeza mishahara bila idhini au ufahamu wa Tume ya Utumishi wa Umma (PSC).
Ruku amesema baadhi ya maafisa wanadaiwa kushirikiana kupanga upandishaji vyeo na nyongeza za mishahara kinyume cha taratibu, huku fedha zilizopatikana kupitia udanganyifu huo zikidaiwa kugawanywa kati ya waliohusika na wafanyakazi walionufaika.
Amewataka wasimamizi wa rasilimali watu, maafisa wa mifumo na watumishi wengine wa umma kuunga mkono mageuzi hayo, akionya kuwa yeyote atakayebainika kuhusika na udanganyifu katika mifumo ya mishahara atawajibishwa.
Waziri huyo pia amewataka watumishi wa umma kuzingatia weledi, uadilifu na uwajibikaji, akisema mwaka ujao utakuwa muhimu kwa uongozi wa nchi na utekelezaji wa ajenda ya maendeleo ya serikali.
"Viongozi wengi wa taasisi mko kwenye ajira za kudumu, lakini mimi na Rais tunapaswa kuhakikisha Wakenya wanapata thamani ya fedha zao ili watupatie mkataba mwingine Agosti 2027," alisema Ruku.
Alikuwa akizungumza katika Shule ya Serikali ya Kenya (KSG), Lower Kabete, Kaunti ya Nairobi, wakati wa mkutano wa Mpango wa Fursa za Utumishi wa Umma na Mafunzo kwa Vitendo (Internship).
Mkutano huo uliwakutanisha wadau wakuu wa serikali kujadili mpango wa kuwaajiri watumishi 50,000 waliokuwa wakihudumu kama wanagenzi, kufuatia agizo la Rais William Ruto.
Mpango huo unalenga kuongeza fursa za ajira kwa vijana huku ukiimarisha uwezo wa rasilimali watu katika taasisi za serikali.
Ruku amesisitiza kuwa taasisi zote lazima zitekeleze agizo la kujiunga na HRIS kabla ya Desemba 20, akionya kuwa wakuu watakaokaidi watawajibishwa.









