Rais William Ruto ametia saini mswada wa akina mama wanaonyonyesha wa mwaka 2024 na kuufanya kuwa sheria, hatua itakayowalazimisha waajiri nchini Kenya kuweka mazingira rafiki kwa wanawake wanaonyonyesha watoto wanapokuwa kazini.
Chini ya sheria hiyo mpya, waajiri watatakiwa kutoa vyumba maalumu vilivyo safi, salama na vya faragha kwa ajili ya akina mama kunyonyesha watoto wao, pamoja na kuwapa mapumziko ya kutosha na ratiba zinazoweza kubadilika kulingana na mahitaji yao.
Sheria hiyo pia inapiga marufuku ubaguzi dhidi ya wanawake kutokana na ujauzito, kujifungua, kunyonyesha au hali nyingine zinazohusiana na uzazi.
Ruto amesema sheria hiyo, iliyodhaminiwa na Mbunge Mteule Sabina Chege, inalenga kulinda haki na utu wa wanawake wanaonyonyesha huku wakiendelea kutekeleza majukumu yao ya kikazi.
"Tunawashukuru wabunge walioiunga mkono kwa kuhakikisha kuwa akina mama wanaweza kulea watoto wao katika mazingira salama na yenye heshima bila kuathiriwa vibaya kutokana na ujauzito, kunyonyesha au kupata watoto," alisema Rais.
Amesema ataagiza mara moja wafanyakazi wa Ikulu kuhakikisha taasisi hiyo inakuwa ya kwanza kutekeleza sheria hiyo kwa kuweka maeneo yanayofaa kwa akina mama wanaonyonyesha.
Aidha, sheria hiyo inazitaka majengo yanayohudumia umma na yenye uwezo wa kupokea watu wasiopungua 50 kuwa na vyumba maalumu vya kubadilishia watoto nepi.
Rais amebainisha kuwa sheria hiyo inalenga kuboresha lishe ya watoto, afya ya akina mama na kuongeza ufanisi kazini kwa kupunguza changamoto zinazowakabili wanawake.
Mswada huo ni miongoni mwa miswada sita ya Bunge la Taifa ambayo Ruto ametia saini kuwa sheria Alhamisi, Novemba 26, katika Ikulu ya Nairobi.
Miongoni mwa mingine ni marekebisho ya Sheria ya Makosa ya Kingono ya mwaka 2023, yanayolenga kuimarisha uzuiaji na utoaji taarifa kuhusu makosa ya kingono kupitia kampeni za elimu kwa umma.
Pia kuna marekebisho ya mwaka 2025 yanayoweka sharti kesi za makosa ya kingono kusikilizwa kupitia mfumo rasmi wa mahakama na kukamilishwa ndani ya miezi sita tangu mshtakiwa kufikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza.
Sheria hiyo pia inapiga marufuku kufutwa kwa kesi kwa msingi wa makubaliano ya nje ya mahakama na kuifanya kuwa kosa kuwatisha au kuwalazimisha waathiriwa kuondoa malalamishi yao.
Miswada mingine iliyotiwa saini inahusu marekebisho ya Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma, kuanzishwa kwa Taasisi ya Wataalamu wa Mazingira nchini Kenya na marekebisho ya Sheria ya Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki.
Ruto amesema hatua hizo zinalenga kuimarisha uwajibikaji, haki na usimamizi wa rasilimali za umma.
Hata hivyo, amesema anatarajia kutia saini pia Mswada wa Ushirikishwaji wa Umma pamoja na miswada saba ya elimu inayolenga kuboresha ufadhili wa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu.









