Polisi katika Kaunti ya Mombasa wameanzisha uchunguzi kufuatia kifo cha mwanamume mmoja aliyefariki katika klabu ya burudani eneo la Kadongo, eneo bunge la Kisauni, katika tukio linalozua maswali kuhusu usalama wa wateja katika maeneo ya starehe.
Marehemu, ambaye alikuwa akifahamika mtaani kwa shughuli za kuchotea na kusambazia wakazi maji, anadaiwa kufariki dunia usiku wa kuamkia Alhamisi baada ya kuanguka ndani ya klabu hiyo muda mfupi baada ya kutoka chooni.
Kwa mujibu wa mashuhuda, mwanamume huyo alikuwa amelewa na alikuwa ameomba ruhusa ya kutumia choo cha klabu hiyo kujisaidia.
Hata hivyo, baada ya kutoka chooni, inadaiwa alianguka ghafla sakafuni na kupoteza maisha katika mazingira ambayo bado hayajafahamika.
Mwili wake ulipelekwa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Mombasa huku maafisa wa polisi wakianza uchunguzi kubaini chanzo cha kifo hicho.
Kifo hicho kinajiri wakati ambapo Mombasa imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali za kiusalama, zikiwemo mashambulizi ya magenge yanayotumia mapanga, visu na marungu kupora na kuwajeruhi wakazi.
Katika maeneo ya Likoni, Changamwe, Kisauni na Bamburi, wakazi wamekuwa wakielezea hofu kufuatia mashambulizi yanayodaiwa kutekelezwa na magenge yanayojulikana kama Panga Boys, huku watu kadhaa wakiripotiwa kujeruhiwa.
Hali hiyo imezua wasiwasi kuhusu usalama wa wakazi wanaofanya shughuli zao nyakati za usiku, wakiwemo wafanyabiashara, waendesha bodaboda na watu wanaotembelea maeneo ya burudani.
Katika tukio jingine, polisi waliwakamata washukiwa wawili katika eneo la Tudor Novemba 23, 2026, wakati wa operesheni iliyowezesha kupatikana kwa silaha za kienyeji zinazodaiwa kutumiwa katika shughuli za uhalifu.
Aidha, Novemba 25, polisi waliwakamata watu watatu katika eneo la Likoni na kurejesha mali zinazoshukiwa kuwa zimeibwa, zikiwemo mitungi ya gesi na simu za mkononi.
Wasiwasi kuhusu usalama pia uliongezeka Oktoba 26 baada ya genge la watu wenye silaha kushambulia kituo cha ukusanyaji ushuru cha kaunti eneo la Likoni, na kumuua afisa mmoja wa serikali ya kaunti huku wengine watatu wakijeruhiwa.
Washambuliaji hao pia waliiba bunduki aina ya AK-47 iliyokuwa na risasi 30 kutoka kwa afisa wa polisi wa utawala.
Kutokana na matukio hayo, maswali yanaendelea kuibuka kuhusu hatua zinazochukuliwa na maafisa wa usalama kudhibiti uhalifu katika maeneo mbalimbali ya Mombasa.
Polisi bado wanatarajiwa kubaini kilichosababisha kifo cha mwanamume huyo wa Kadongo, huku uchunguzi ukiendelea.









