Mahakama moja mjini Nakuru imewapata maafisa wawili wa Shirika la Huduma za Wanyamapori nchini (KWS) na hatia ya kumteka nyara mvuvi Brian Odhiambo, ambaye alitoweka katika mazingira tatanishi Januari 2025.

Maafisa hao ni Senior Sergeant Francis Wachira na dereva Abdulrahman Ali Sudi, ambao walikuwa miongoni mwa maafisa sita wa KWS walioshtakiwa kuhusiana na kutoweka kwa Odhiambo baada ya kudaiwa kukamatwa karibu na Ziwa Nakuru.

Akitoa uamuzi huo Alhamisi, Novemba 26, 2026, Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Nakuru, Kipkurui Kibelion, alisema upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha kesi yake dhidi ya maafisa hao wawili bila kuacha shaka yoyote.

Hata hivyo, mahakama iliwaachilia huru maafisa wengine wanne wa KWS waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka hayo.

Maafisa walioachiliwa ni Alexander Lorogoi, Isaac Ochieng Odhiambo, Michael Wabukala na Evans Kimaiyo Kipsang.

Kesi hiyo inahusiana na kutoweka kwa Odhiambo mnamo Januari 18, 2025, baada ya kudaiwa kukamatwa na maafisa wa KWS wakati wa operesheni iliyolenga kukabiliana na shughuli za uvuvi haramu na uvamizi katika eneo la Hifadhi ya Kitaifa ya Ziwa Nakuru.

Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani, Odhiambo alikamatwa katika eneo la Manyani kabla ya kuhamishwa na maafisa hao katika magari tofauti.

Katika utetezi wake, Sudi aliambia mahakama kwamba alikuwa ameachwa kumlinda mshukiwa aliyekuwa amekamatwa, lakini baadaye alitoroka baada ya kuomba ruhusa kwenda kujisaidia.

Hata hivyo, maelezo hayo yaliibua maswali wakati wa kuhojiwa na upande wa mashtaka, hasa kuhusu namna mtu aliyedaiwa kuwa dhaifu na aliyechoka alivyoweza kumshinda afisa huyo na kutoroka.

Mahakama pia ilisikiliza ushahidi kuhusu mawasiliano ya simu na mienendo ya maafisa hao siku ambayo Odhiambo alitoweka.

Licha ya hukumu hiyo, mwili wa Odhiambo haujapatikana hadi sasa, na familia yake bado haina majibu kuhusu kilichompata baada ya kukamatwa kwake.

Hata hivyo, hakimu alibainisha kuwa kutopatikana kwa mwili wa Odhiambo hakumaanishi kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kosa, kwa kuwa maafisa hao walikuwa wakishtakiwa kwa utekaji nyara na si mauaji.

Mahakama imepanga kutaja kesi hiyo Desemba 2, 2026, kwa ajili ya kusikiliza hoja za kupunguziwa adhabu kabla ya kutoa maelekezo kuhusu hukumu dhidi ya maafisa hao wawili.