Nchi ya Eritrea imeandika historia katika mapambano dhidi ya upofu unaosababishwa na maambukizi ya macho, baada ya kufanikiwa kuondoa ugonjwa wa trachoma kama tatizo la afya ya umma, hatua ambayo imepongeza na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Mafanikio hayo yanaashiria ushindi mkubwa kwa wananchi wa Eritrea na jumuiya ya kimataifa katika juhudi za kupambana na magonjwa yanayoweza kuzuilika, lakini ambayo yameendelea kuhatarisha afya na maisha ya mamilioni ya watu duniani.

WHO imepongeza hatua hiyo, ikiitaja kuwa mafanikio muhimu ya afya ya umma, huku Eritrea ikiungana na mataifa mengine yaliyofanikiwa kudhibiti ugonjwa huo kupitia juhudi za muda mrefu za afya na kinga.

Trachoma ni ugonjwa wa macho unaosababishwa na bakteria Chlamydia trachomatis, na unaendelea kuwa chanzo kikuu cha upofu unaotokana na maambukizi duniani.

Ugonjwa huo huenea kupitia kugusana na majimaji kutoka machoni au puani mwa mtu aliyeambukizwa, pamoja na matumizi ya vitu vilivyochafuliwa na majimaji hayo.

Maambukizi ya mara kwa mara yanaweza kusababisha makovu ndani ya kope, hali inayoweza kufanya kope kujikunja kuelekea ndani na nyusi kukwaruza sehemu ya mbele ya jicho.

Hali hiyo, inayojulikana kama trachomatous trichiasis, inaweza kusababisha maumivu makali, uharibifu wa konea na hatimaye upofu usioweza kurekebishwa iwapo haitatibiwa.

Katika ushindi huo, Eritrea imeonyesha kuwa mapambano dhidi ya magonjwa yanayoweza kusababisha ulemavu wa kudumu yanaweza kufanikiwa kupitia mikakati madhubuti ya afya ya umma na ushirikiano wa jamii.

WHO inahimiza mataifa yanayokabiliwa na trachoma kuimarisha juhudi za kuzuia maambukizi, kutibu wagonjwa na kuboresha mazingira ya usafi ili kupunguza maambukizi mapya.

Mkakati wa WHO wa SAFE unahusisha upasuaji kwa wagonjwa walioathiriwa na hatua za ugonjwa, matumizi ya antibiotiki, usafi wa uso na kuboresha mazingira, ikiwemo upatikanaji wa maji safi na huduma za vyoo.

Mafanikio ya Eritrea yanakuja wakati dunia ikiendelea na juhudi za kuondoa trachoma kama tatizo la afya ya umma ifikapo mwaka 2030, chini ya mpango wa WHO wa kukabiliana na magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika.

Hata hivyo, kuondoa ugonjwa kama tatizo la afya ya umma hakumaanishi kuwa maambukizi mapya hayawezi kutokea. Nchi zinahitajika kuendelea na ufuatiliaji, kutambua wagonjwa mapema na kuhakikisha huduma za matibabu zinapatikana.

Ushindi wa Eritrea ni ujumbe muhimu kwa mataifa mengine kwamba upofu unaotokana na trachoma unaweza kuzuilika, na kwamba uwekezaji katika afya, usafi na elimu ya jamii unaweza kubadilisha maisha ya mamilioni ya watu.