Bunge la Senegal limepitisha azimio la kupinga uamuzi wa Rais wa nchi hiyo wa kuanza kutekeleza bajeti ya serikali, hatua inayozidisha mvutano kati ya mhimili wa utendaji na chombo cha kutunga sheria nchini humo.

Azimio hilo linaashiria kutokubaliana kwa wabunge na hatua ya Rais ya kuendelea na utekelezaji wa bajeti licha ya kuwepo kwa pingamizi kuhusu mchakato huo.

Katika kura iliyofanyika Jumatano, Novemba 25, wabunge 128 waliunga mkono azimio hilo huku tisa wakilipinga, hatua inayoongeza mgogoro wa kisiasa kuhusu usimamizi wa fedha za umma.

Rais Bassirou Diomaye Faye wiki iliyopita alitangaza kuwa atatekeleza marekebisho ya bajeti ya mwaka 2026 kupitia amri ya rais, baada ya wabunge kukataa pendekezo hilo Novemba 3.

Uamuzi huo umemweka katika mzozo na aliyekuwa Waziri Mkuu wake, Ousmane Sonko, ambaye kwa sasa anaongoza Bunge la Taifa la Senegal.

Chama cha Pastef kinachoongozwa na Sonko ndicho chenye wingi wa wabunge katika Bunge la Taifa na kimekuwa kikipinga marekebisho ya bajeti ya mwaka 2026 pamoja na mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2027.

Kabla ya azimio hilo kupitishwa, wabunge wa Pastef walidai serikali imeshindwa kutoa maelezo ya kutosha kuhusu hali halisi ya fedha za umma na makadirio ya madeni yaliyotumika kuandaa bajeti iliyorekebishwa.

Kwa upande wake, Faye ametetea uamuzi wake akisema alichukua hatua hiyo kwa kuzingatia wajibu wake wa kuhakikisha serikali inaendelea kutekeleza majukumu yake na shughuli za taifa haziathiriki.

Mvutano huo pia unaweka hatarini mpango wa ufadhili wa dola bilioni 2.2 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ambao ni muhimu katika juhudi za Senegal kurekebisha hali yake ya kifedha na kushughulikia mzigo mkubwa wa madeni.

Mpango huo wa miaka mitatu ulikuwa umefikia makubaliano ya awali kati ya serikali na IMF, lakini bado unasubiri kuidhinishwa na bodi ya utendaji ya shirika hilo.

Senegal imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa za kifedha tangu mwaka 2024, wakati serikali ilipobaini kuwa utawala uliotangulia ulikuwa haujaripoti kwa usahihi kiwango cha deni la taifa, ambalo wachambuzi walilikadiria kuwa lilikuwa limefichwa kwa takriban dola bilioni 13.

Mchambuzi wa masuala ya uwekezaji katika benki ya Morgan Stanley, Neville Mandimika, ameonya kuwa mkwamo huo wa bajeti unaweza kuhatarisha mipango ya kifedha ya Senegal katika kipindi cha kati.

Mandimika alisema itakuwa vigumu kwa nchi hiyo kukamilisha mchakato wa kurekebisha madeni yake ifikapo mwisho wa mwaka 2026.

Hata hivyo, mvutano kati ya Faye na Sonko unaendelea kuibua maswali kuhusu mustakabali wa ushirikiano wao wa kisiasa, huku pande zote zikionekana kutofautiana kuhusu namna ya kusimamia uchumi wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.