Takriban watu 31 wamefariki dunia na wengine 21 kujeruhiwa baada ya lori lililokuwa limebeba mafuta kupinduka na kusababisha moto mkubwa kwenye barabara kuu ya Ring Road jijini Cairo, nchini Misri.
Ajali hiyo ilitokea Jumatano jioni katika eneo la Al-Warraq, lililopo katika kaunti ya Giza, sehemu ya jiji kuu la Greater Cairo, huku moto ukisambaa kwa kasi na kuteketeza magari kadhaa yaliyokuwa yakipita katika barabara hiyo yenye shughuli nyingi.
Kwa mujibu wa mamlaka za afya nchini Misri, moto huo ulisababisha uharibifu mkubwa, huku zaidi ya magari na pikipiki 27 yakiteketea baada ya lori hilo kuripotiwa kupinduka na kumwaga mafuta yaliyokuwa yakisafirishwa.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema moto ulienea kwa haraka na kuwafanya baadhi ya madereva na abiria kushindwa kujinasua kutoka kwenye magari yao yaliyokuwa yamezingirwa na miali ya moto.
Timu za uokoaji na zimamoto zilipelekwa eneo la tukio, huku waokoaji wakionekana wakijitahidi kuwatoa watu waliokuwa wamenasa ndani ya magari yaliyokuwa yakiwaka moto.
Wizara ya Afya ya Misri ilisema kuwa majeruhi walipelekwa katika hospitali mbalimbali za karibu kwa matibabu, huku baadhi yao wakiripotiwa kujeruhiwa vibaya kutokana na kuungua na kuvuta moshi.
Jumla ya magari 39 ya kubeba wagonjwa yalitumwa kusaidia shughuli za uokoaji na kuwahamisha walioathirika katika ajali hiyo.
Wakati huo huo, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu nchini humo imeanzisha uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo pamoja na mazingira yaliyochangia kutokea kwa mkasa huo.
Mamlaka pia zimeagiza vipimo vya vinasaba vya DNA kufanyika ili kusaidia kutambua miili ya baadhi ya waliofariki ambayo iliharibiwa vibaya na moto.
Rais wa Misri, Abdel Fattah al-Sisi, ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao, huku akielekeza mamlaka husika kuhakikisha majeruhi wanapata msaada unaohitajika.
Idadi ya waliofariki imetajwa kuwa ya awali, huku kukiwa na hofu kwamba huenda ikaongezeka kutokana na hali ya baadhi ya majeruhi.
Tukio hilo limeibua tena wasiwasi kuhusu usalama wa barabarani nchini Misri, ambako ajali za magari zimekuwa zikisababisha vifo vya maelfu ya watu kila mwaka.
Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa watu 5,829 walifariki katika ajali za barabarani nchini humo mwaka 2025, huku mwendo kasi, hali duni ya barabara na kutotekelezwa ipasavyo kwa sheria za trafiki zikitajwa kuwa miongoni mwa sababu kuu za ajali hizo.









