Takriban watu 17 wameuawa katika mashambulizi mawili tofauti ya kutumia bunduki yaliyotokea ndani ya siku moja nchini Afrika Kusini.
Aidha polisi wameendelea kuchunguza uwezekano wa moja ya matukio hayo kuhusishwa na mauaji ya watu 12 yaliyotokea mwaka jana.
Mashambulizi hayo yalitokea Jumapili, Novemba 15, katika maeneo ya Sweetwaters, nje ya mji wa Pietermaritzburg, na Jeffsville, makazi yasiyo rasmi yaliyoko karibu na mji mkuu wa kiutawala wa nchi hiyo, Pretoria.
Katika tukio la kwanza, watu wanane walikutwa wamefariki ndani ya gari lililokuwa limejaa matundu ya risasi katika eneo la Sweetwaters.
Polisi walisema hadi Jumatatu walikuwa bado hawajathibitisha utambulisho wa waathiriwa wala kubaini waliohusika na shambulizi hilo. Hata hivyo, baadhi ya familia zilikuwa zimejitokeza kusaidia katika zoezi la kuwatambua ndugu zao.
Msemaji wa polisi, Robert Netshiunda, anasema uchunguzi ulikuwa katika hatua za awali na kwamba ilikuwa mapema kubaini sababu za mauaji hayo au watu waliohusika.
Katika shambulizi la pili, watu tisa, wakiwemo wanaume sita na wanawake watatu, walipigwa risasi na kuuawa ndani ya nyumba moja yenye vyumba vinne katika makazi ya Jeffsville, karibu na Pretoria.
Kwa mujibu wa msemaji wa polisi wa Gauteng, Brenda Muridili, maafisa walipokea taarifa kuhusu tukio hilo mwendo wa saa 1:30 asubuhi Jumatatu, Novemba 16, na walipofika eneo la tukio walikuta miili ya waathiriwa ikiwa na majeraha ya risasi.
Inaaminika kuwa shambulizi hilo lilitekelezwa kati ya saa nne na saa tano usiku wa Jumapili. Hakuna mshukiwa aliyekuwa amekamatwa kufikia wakati polisi walipokuwa wakitoa taarifa kuhusu tukio hilo.
Kamishna wa Polisi katika jimbo la Gauteng, Tommy Mthombeni, alisema wachunguzi hawaondoi uwezekano wa mauaji hayo kuhusishwa na shambulizi jingine lililotokea mwaka jana katika makazi ya Saulsville, karibu na eneo hilo.
Katika tukio hilo, watu 12 waliuawa huku wengine 13 wakijeruhiwa. Mthombeni alisema mmoja wa waliouawa katika shambulizi la Jeffsville alikuwa mtu aliyekuwa akichunguzwa kuhusiana na mauaji ya Saulsville.
Alisema polisi wanachunguza uwezekano kuwa shambulizi hilo lilikuwa la kulipiza kisasi, ingawa hakuna uhusiano uliokuwa umethibitishwa rasmi.
Matukio hayo yanaongeza wasiwasi kuhusu ongezeko la mashambulizi ya kutumia silaha nchini Afrika Kusini, ambako baadhi ya mauaji ya halaiki yamehusishwa na magenge ya uhalifu, migogoro ya biashara haramu na mapambano ya kudhibiti maeneo.
Miongoni mwa matukio ya hivi karibuni ni shambulizi lililotokea Septemba karibu na Durban, ambapo watu wasiopungua 11, akiwemo mwanamke mjamzito, waliuawa wakati watu wenye silaha walipovamia nyumba iliyokuwa na mkusanyiko wa watu.
Polisi wanaendelea na uchunguzi wa mashambulizi hayo mawili huku wakisaka waliohusika na kubaini sababu za umwagaji damu huo.









