Wahadhiri Watishia Kurejelea Mgomo, Waitaka Serikali Kulipa Madeni

Chama cha wafanyakazi wa vyuo vikuu nchini (UASU) kinaonya kuwa kinaweza kurejelea mgomo iwapo serikali haitashughulikia madai ambayo bado hayajatatuliwa, licha ya mazungumzo yanayoendelea kati ya pande hizo.

Katibu Mkuu wa UASU, Constantine Wasonga, anasisitiza kuwa serikali inapaswa kulipa madeni inayodaiwa na wahadhiri na kuhakikisha kuwa masuala yaliyoibua mizozo katika sekta ya elimu ya juu yanapatiwa suluhu ya kudumu.

Akizungumza mbele ya kamati za pamoja za Bunge la Kitaifa zinazoshughulikia masuala ya Leba na Elimu, Wasonga anahoji pia mpango wa kulipa mishahara ya wahadhiri kupitia ada zinazolipwa na wanafunzi.

Anasema utaratibu huo unazua maswali kuhusu namna vyuo vikuu vinavyotekeleza wajibu wao wa kuwalipa wafanyakazi, akitaka Bunge kuingilia kati na kuhakikisha kuwa suala hilo linapatiwa ufumbuzi.

Wasonga anatahadharisha kuwa iwapo serikali haitatimiza makubaliano yaliyopo na kushughulikia malalamishi ya wahadhiri, huenda wafanyakazi hao wakalazimika kurejelea mgomo ili kushinikiza madai yao yatimizwe.

Anaitaka serikali kuonyesha dhamira ya kweli katika kutekeleza makubaliano na kuepusha hali inayoweza kuvuruga shughuli za masomo katika vyuo vikuu nchini.

Kwa upande wake, Katibu katika Wizara ya Leba, Shadrack Mwadime, anasema serikali iko tayari kuhakikisha kuwa makubaliano yaliyofikiwa na wahadhiri yanatekelezwa kikamilifu.

Mwadime anasema mazungumzo yanaendelea kuhusu masuala mengine ambayo bado yanazua utata kati ya serikali na wahadhiri, akidokeza kuwa juhudi zinaendelea kutafuta suluhu kabla ya Februari mwaka ujao.

Anasisitiza kuwa serikali inalenga kuhakikisha kuwa masuala yaliyosalia yanatatuliwa kupitia mazungumzo, badala ya kuruhusu tofauti hizo kuathiri shughuli za vyuo vikuu.

Kauli za viongozi hao zinajiri huku kukiwa na msukumo wa kuhakikisha kuwa makubaliano kati ya serikali na wahadhiri yanatekelezwa, ili kuzuia uwezekano wa mgomo mwingine ambao unaweza kuathiri kalenda ya masomo na shughuli za kitaaluma katika taasisi za elimu ya juu.

Hata hivyo, onyo la UASU linaonyesha kuwa suala la madeni na utaratibu wa ufadhili wa mishahara ya wahadhiri bado ni miongoni mwa changamoto zinazohitaji kushughulikiwa ili kuhakikisha utulivu unadumishwa katika vyuo vikuu nchini.