Mahakama Kuu imewaamuru maafisa wakuu wa usalama nchini kuwasilisha mbele yake wakili wa Nairobi Abshir Ahmedsadak Abdi, akiwa hai au amefariki, kufikia saa 8:30 mchana leo, Jumatano, Novemba 4, 2026.
Agizo hilo limetolewa na Jaji Alexander Muteti, anayehudumu kama jaji wa zamu katika Kitengo cha Makosa ya Jinai cha Mahakama Kuu, baada ya kuthibitisha kuwa ombi lililowasilishwa kuhusu kutoweka kwa wakili huyo ni la dharura na linahitaji kusikilizwa mara moja.
Katika uamuzi wake, Jaji Muteti amewaagiza walalamikiwa kuhakikisha Abshir anafikishwa mahakamani bila kujali hali yake ya sasa, akisisitiza kuwa lazima wawasilishe mwili wake mbele ya mahakama katika muda uliowekwa.
Mahakama pia imewaita binafsi Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja pamoja na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Mohammed Amin, kufika mbele yake au kupitia mawakili wao walioteuliwa rasmi.
Viongozi hao wa usalama wanatakiwa kueleza mazingira yaliyosababisha kukamatwa na kuzuiliwa kwa Abshir, huku wakiwasilisha hati zozote za kukamatwa kwake iwapo zilitolewa kisheria.
Aidha, wanapaswa kuonyesha sababu zinazofanya wakili huyo asiweze kuachiliwa mara moja kutoka kizuizini, endapo atathibitika kuwa chini ya ulinzi wa vyombo vya usalama.
Agizo hilo limewahusu Inspekta Jenerali wa Polisi, Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) pamoja na mashirika mengine ya usalama ambayo yameorodheshwa kama walalamikiwa katika kesi hiyo.
Mahakama imeelekeza kuwa maombi pamoja na nakala za maagizo hayo yawasilishwe kwa walalamikiwa wote ili kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika mara moja.
Kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa katika kikao cha wazi cha mahakama saa 8:30 mchana, huku ikisubiriwa kujulikana iwapo vyombo vya usalama vitamwasilisha wakili huyo na kueleza walichokijua kuhusu kutoweka kwake.
Abshir, ambaye ni wakili wa Mahakama Kuu na anayefanya kazi katika kampuni ya mawakili ya Abshir & Njagi Advocates iliyoko Kilimani, anadaiwa kutekwa nyara Oktoba 31, 2026, kando ya barabara ya Muchai jijini Nairobi.
Kutoweka kwake kulizua wasiwasi baada ya gari lake aina ya Toyota lenye nambari za usajili KDL 356C kupatikana likiwa limeachwa katika eneo hilo, huku mahali alipo pakibaki kutofahamika.
Kesi hiyo sasa inaweka shinikizo kwa viongozi wa vyombo vya usalama kutoa maelezo kuhusu mahali alipo wakili huyo na mazingira ya kutoweka kwake.









