Kutoka Nairobi Hadi Mwanza: Safari Ya Mapenzi Ya Charlene Ruto
Macho ya Wakenya na Watanzania yanaelekezwa jijini Mwanza, Tanzania, ambako binti wa Rais wa Kenya William Ruto, Charlene Ruto, anadaiwa kuwa anajiandaa kufunga ndoa na mchumba wake, Isaya Yunge, mfanyabiashara kutoka Tanzania.
Inadaiwa kuwa harusi hiyo itafanyika Ijumaa, Novemba 6, 2026, katika ufukwe wa Malaika Beach Resort jijini Mwanza, huku maandalizi ya hafla hiyo yakiripotiwa kuanza kushika kasi.
Sherehe hiyo inadaiwa kuvutia wageni mashuhuri kutoka Kenya na Tanzania, wakiwemo viongozi wa kisiasa na watu wenye ushawishi katika jamii. Rais William Ruto pia anatarajiwa kuhudhuria hafla hiyo ya kifamilia, iwapo mipango hiyo itathibitishwa.
Charlene, ambaye ni mmoja wa watoto wa Rais William Ruto na Mama wa Taifa Rachel Ruto, amejijengea utambulisho wake kupitia shughuli za kuwawezesha vijana, ujasiriamali na utunzaji wa mazingira.
Mbali na kuwa binti wa kiongozi wa taifa, Charlene amekuwa akishiriki katika majukwaa mbalimbali ya kitaifa na kimataifa yanayohusu vijana na maendeleo ya jamii. Ana taaluma ya mawasiliano kutoka Chuo Kikuu cha Daystar na shahada ya uzamili katika usimamizi wa biashara ya ukarimu kutoka Les Roches nchini Uswisi.
Kwa upande wake, Isaya Yunge ni mfanyabiashara wa teknolojia kutoka Tanzania, anayehusishwa na SomaApp, jukwaa la kidijitali linalolenga kuwaunganisha wanafunzi wa Afrika na fursa za ufadhili wa masomo.
Safari ya wawili hao kuelekea ndoa ilipiga hatua muhimu Agosti 8, 2026, walipofanya sherehe ya mahari na kuvishana pete ya uchumba katika eneo la Kilgoris, Kaunti ya Narok nchini Kenya.
Hafla hiyo ya kitamaduni iliwaunganisha wanafamilia kutoka pande zote mbili, huku shamrashamra, nyimbo na ngoma za kitamaduni zikiashiria hatua mpya katika uhusiano wao.
Iwapo taarifa kuhusu harusi ya Mwanza zitathibitishwa, tukio hilo litakuwa sura nyingine muhimu katika safari ya wawili hao, huku muungano wao ukitarajiwa kuunganisha familia kutoka mataifa mawili jirani ya Afrika Mashariki.
Kwa sasa, macho yanaelekezwa Mwanza kusubiri iwapo madai kuhusu tarehe na mahali pa harusi hiyo yatatimia na kuwapa watu burudsni ya muziki na hata lishe.









