Mwanasiasa mwenye asili ya Kenya, Huldah Momanyi-Hiltsley, amepata ushindi mwingine wa kisiasa nchini Marekani baada ya kuchaguliwa tena kuwa mwakilishi katika Bunge la Jimbo la Minnesota, na hivyo kuendeleza safari yake ya uongozi katika taifa hilo la Amerika Kaskazini.

Matokeo ya awali yaliyotolewa na ofisi ya Katibu wa Jimbo la Minnesota Jumatano, Novemba 4, 2026, yanaonyesha kuwa Momanyi-Hiltsley alipata kura 9,852, sawa na asilimia 71.8 ya kura zote zilizopigwa katika eneo la uchaguzi la District 38A.

Mpinzani wake kutoka chama cha Republican, Charlie Kistler, alipata kura 3,840, ambazo ni asilimia 28 ya kura zilizopigwa.

Ushindi huo unamuwezesha Momanyi-Hiltsley kuhifadhi kiti chake kwa muhula mwingine wa miaka miwili, unaotarajiwa kuanza Januari 2027, baada ya matokeo hayo kuthibitishwa rasmi.

Eneo la uchaguzi la District 38A linajumuisha mji wa Osseo pamoja na sehemu za Brooklyn Park, jimbo la Minnesota.

Kabla ya kufungwa kwa vituo vya kupigia kura, mwanasiasa huyo alikuwa amewashukuru wafuasi wake na wote waliojitokeza kushiriki katika mchakato wa uchaguzi, akisema alikuwa na shukrani kwa mchango wao bila kujali matokeo.

Kupitia ujumbe wake, alisema uchaguzi huo ulikuwa sehemu ya jitihada za kulinda demokrasia na kutambua mchango wa kila mmoja aliyeshiriki katika kampeni zake.

Momanyi-Hiltsley aliingia katika historia mwaka 2024 baada ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuwakilisha District 38A katika Bunge la Minnesota, akiwa mwanamke wa kwanza mwenye asili ya Kenya kuchaguliwa katika nafasi hiyo na mhamiaji wa kwanza aliyezaliwa Kenya kushikilia wadhifa wa kuchaguliwa katika ngazi ya jimbo nchini Marekani.

Akiwa mwanachama wa chama cha Democratic-Farmer-Labor (DFL), kinachohusishwa na chama cha Democratic nchini Marekani, amekuwa akijikita katika masuala ya upatikanaji wa huduma za afya, haki za uzazi, udhibiti wa umiliki wa bunduki na upatikanaji wa makazi bora.

Safari yake ya kisiasa haikuwa rahisi kila wakati. Mwaka 2022, alijaribu kuwania kiti cha Seneti ya Jimbo la Minnesota katika eneo la District 38 kupitia chama hicho, lakini hakufanikiwa. Hata hivyo, aliendelea na juhudi zake za kisiasa hadi aliposhinda uchaguzi wa 2024.

Asili na Safari ya Maisha

Momanyi-Hiltsley ni binti wa Philip Momanyi na Tabitha Momanyi, wazazi wenye asili ya Kaunti ya Nyamira nchini Kenya ambao walihamia Marekani kutafuta maisha bora.

Alitumia miaka yake ya awali nchini Kenya pamoja na ndugu zake wawili kabla ya kuhamia Marekani kuungana na wazazi wake. Baba yake alihamia nchini humo kwanza, akifuatiwa na mama yake mwaka 1992, huku Huldah na ndugu zake wakijiunga nao Minnesota mwaka 1995 akiwa na umri wa takriban miaka tisa.

Alianza safari yake ya elimu nchini Kenya katika Shule ya Msingi ya Nyambaria kabla ya kuendelea na masomo nchini Marekani katika Shule ya Upili ya Robbinsdale Cooper iliyoko New Hope, Minnesota, ambako alihitimu mwaka 2004.

Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Bethel, ambako alipata shahada tatu za kwanza katika biashara ya kimataifa, mahusiano ya kimataifa na masomo ya maridhiano. Pia alipata shahada ya uzamili katika usimamizi wa biashara duniani (MBA).

Kabla ya kuingia katika siasa, Momanyi-Hiltsley alifanya kazi katika sekta ya kampuni binafsi katika maeneo ya uzingatiaji wa sheria na kanuni za biashara, faragha ya taarifa na ulinzi wa data.

Pia amekuwa akishiriki katika shughuli za kijamii na uongozi wa jamii ya Wakenya nchini Marekani, akiwahi kuwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kuwa rais wa shirika la Mwanyagetinge, linalohusishwa na jamii ya Wakisii.

Momanyi-Hiltsley ameolewa na Bart Hiltsley, na wamejaliwa watoto wawili, Jaydah Rae na Jordan Philip. Familia hiyo inaishi Brooklyn Park, Minnesota.

Ushindi wake wa pili mfululizo unaendeleza uwakilishi wake katika siasa za Marekani na kuongeza idadi ya Wakenya wenye asili ya Afrika Mashariki wanaoshikilia nyadhifa za uongozi katika mataifa ya kigeni.