Mchungaji mwenye utata Paul Nthenge Mackenzie amehukumiwa kifungo cha miaka 200 gerezani kutokana na mauaji ya watu 191, wakiwemo watoto 190, katika msitu wa Shakahola, kaunti ya Kilifi.

Hukumu hiyo imetolewa Ijumaa Novemba 6, 2026, na Jaji wa Mahakama Kuu ya Mombasa Diana Kavedza Mochache, baada ya Mackenzie kupatikana na hatia ya makosa 191 ya mauaji miezi kadhaa iliopita.

Mackenzie, ambaye alikuwa akiongoza kanisa la Good News International, alishtakiwa kwa kuwalaghai wafuasi wake kwa mafundisho ya kidini yaliyowahimiza kufunga kula hadi kufa wakiamini wangekutana na Yesu mbinguni.

Katika uamuzi wake wa awali, mahakama ilibaini kuwa Mackenzie alikuwa na jukumu kuu katika kuhamisha wafuasi wake hadi eneo la mbali la Shakahola na kuwaelekeza kufunga hadi kufariki.

Jaji Kavedza alisema Mackenzie alikuwa na jukumu kubwa la jinai katika vifo hivyo, akitumia mafundisho ya kidini kuendesha mfumo wa kufunga uliosababisha vifo vya watoto na watu wazima.

Upande wa mashtaka ulikuwa umeiomba mahakama kumpa Mackenzie hukumu ya kifo, ukisema ukubwa wa mauaji hayo na ukatili uliohusika vilistahili adhabu kali zaidi inayotolewa na sheria.

Hata hivyo, mahakama imeamua kumhukumu kifungo cha miaka 200 jela badala ya adhabu ya kifo.

Mackenzie alihukumiwa pamoja na washirika wake 28, ambao pia walipatikana na hatia ya makosa 191 ya mauaji katika uamuzi uliotolewa Oktoba 19, 2026.

Wengine walihusishwa na kutekeleza maagizo ya kufunga, kuwazuia wafuasi waliotaka kuacha, pamoja na kuficha miili ya waliokuwa wamefariki.

Sakata la Shakahola lilishtua Kenya mwaka 2023 baada ya polisi na wachunguzi kugundua makaburi ya halaiki katika msitu huo, huku mamia ya miili ikifukuliwa.

Zaidi ya miili 400 ilipatikana katika operesheni za uchunguzi, ingawa ni vifo 191 vilivyokuwa sehemu ya kesi hii ya mauaji.

Mackenzie na washirika wake walikuwa wakikabiliwa na ushahidi wa mashahidi, wataalamu wa uchunguzi wa maiti na manusura wa Shakahola.

Hukumu hiyo ni hatua muhimu katika moja ya kesi kubwa zaidi za mauaji na misimamo mikali ya kidini nchini Kenya.

Mackenzie pia anakabiliwa na kesi nyingine zinazohusiana na ugaidi, itikadi kali na makosa dhidi ya watoto, ambazo zinaendelea kando na kesi hii ya mauaji.