Matumizi mabaya ya tembe za dharura za kuzuia mimba maarufu kama Postinor-2 (P2) miongoni mwa vijana nchini Kenya yameibua wasiwasi miongoni mwa wataalamu wa afya, huku kukiwa na wito wa kuongeza elimu kuhusu afya ya uzazi na matumizi sahihi ya njia za kupanga uzazi.
Kwa mujibu wa ripoti, baadhi ya vijana wamekuwa wakizitumia tembe hizo mara kwa mara baada ya kushiriki ngono bila kinga, badala ya kuzingatia njia za kawaida za uzazi wa mpango zinazotoa kinga endelevu dhidi ya mimba zisizotarajiwa.
P2 ni tembe za dharura zinazotumika kuzuia mimba baada ya kushiriki ngono bila kinga au pale ambapo njia iliyotumika ya uzazi wa mpango imeshindwa.
Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa tembe hizo hazipaswi kuchukuliwa kama mbadala wa njia za kawaida za kupanga uzazi, hasa kwa watu wanaoshiriki ngono mara kwa mara.
Miongoni mwa changamoto zinazohusishwa na matumizi ya mara kwa mara ya P2 ni kuvurugika kwa mzunguko wa hedhi, kutokwa na damu kusiko kwa kawaida, kichefuchefu na maumivu ya kichwa.
Baadhi ya vijana pia wanakosa taarifa sahihi kuhusu namna tembe hizo zinavyofanya kazi, muda unaofaa kuzitumia na kiwango cha ufanisi wake katika kuzuia mimba.
Katika ripoti hiyo, mwanamke mmoja aliyetambulishwa kwa jina la Ann, ambalo si jina lake halisi, alieleza jinsi alivyopata ujauzito licha ya kutumia P2 baada ya kushiriki ngono bila kinga.
Alisema alikuwa amezoea kutumia tembe hizo kila aliposhiriki ngono bila kinga, lakini hatimaye akapata ujauzito licha ya kuzitumia.
Daktari Margarete Wamucii wa Hospitali ya Level Five ya Embu alisisitiza umuhimu wa watu wanaoshiriki ngono mara kwa mara kutumia njia za kawaida za kupanga uzazi badala ya kutegemea P2.
Alisema vijana wanapaswa kupewa elimu kuhusu njia mbalimbali za uzazi wa mpango ili waweze kufanya maamuzi sahihi kuhusu afya yao ya uzazi.
Wakati huohuo, mjadala kuhusu matumizi mabaya ya dawa nchini umeongezeka baada ya Pharmacy and Poisons Board kutoa tahadhari kuhusu matumizi ya dawa ya Cetirizine kwa madai ya kubana uke au kusababisha ukavu.
Bodi hiyo imefafanua kuwa Cetirizine ni dawa ya kutibu mzio na haijathibitishwa kisayansi kutumika kwa ajili ya kubana uke. Matumizi yake nje ya maelekezo ya kitabibu yanaweza kusababisha madhara.
Wataalamu wanataka Wakenya kuacha kufuata mitindo ya matumizi ya dawa inayosambaa mitandaoni na badala yake kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya.









