Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limeonya kuhusu kuongezeka kwa vitisho dhidi ya wanahabari duniani, likisema karibu waandishi wa habari tisa kati ya kumi wanaouawa hawapati haki huku wahusika wa mauaji hayo wakikwepa kuwajibishwa.

Onyo hilo limetolewa Jumatatu, Novemba 2, 2026, wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Kutoadhibiwa kwa Uhalifu Dhidi ya Waandishi wa Habari.

Katika ripoti yake kuhusu usalama wa wanahabari na kutoadhibiwa kwa wahusika wa uhalifu dhidi yao, UNESCO imesema waandishi 189 wa habari waliuawa katika kipindi cha miaka miwili ya 2024 na 2025, huku asilimia 67 ya mauaji hayo yakitokea katika maeneo yenye migogoro ya kivita.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa kiwango cha kutoadhibiwa kwa mauaji ya wanahabari duniani kimefikia asilimia 86, ongezeko la asilimia moja ikilinganishwa na tathmini iliyopita.

Hii ina maana kuwa karibu mauaji tisa kati ya kumi ya wanahabari bado hayajatatuliwa katika mifumo ya mahakama, hali inayozua wasiwasi kuhusu usalama wa wale wanaofichua ukweli na kuisimamia jamii.

UNESCO imesema teknolojia mpya na silaha zinazotumiwa katika vita zimebadili namna wanahabari wanavyolengwa, huku matumizi ya ndege zisizo na rubani yakiongeza hatari kwa waandishi wanaoripoti kutoka maeneo ya mapigano.

Katika kipindi hicho, wanahabari 50 waliuawa kwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika maeneo sita ya vita, jambo linaloashiria mabadiliko makubwa katika vitisho vinavyowakabili wanahabari.

Wanawake wanahabari pia wanakabiliwa na hatari zinazoongezeka za unyanyasaji wa kijinsia, mashambulizi ya mitandaoni na vitisho vinavyolenga kuwanyamazisha.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameitaka dunia kuhakikisha kila shambulizi dhidi ya wanahabari linachunguzwa, wahusika wanakabiliwa na sheria na mashambulizi ya mitandaoni yanakomeshwa.

Guterres amesema wanahabari wana jukumu muhimu la kuhabarisha umma na kuwawajibisha viongozi, lakini mara nyingi wanakabiliwa na vitisho, ufuatiliaji, mashambulizi, vifungo na hata mauaji kwa sababu ya kazi zao.

Katika maeneo yenye migogoro ya kivita, kiwango cha kutoadhibiwa kwa wahusika wa mauaji ya wanahabari kinakaribia asilimia 100.

Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu “Vitisho Vinabadilika, Kutoadhibiwa Kunaendelea”, inayolenga kuhamasisha serikali, vyombo vya habari na jamii kuimarisha mifumo ya ulinzi na uwajibikaji.

Siku hiyo ilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2013 kupitia azimio lililotaka mataifa kuchukua hatua madhubuti kukomesha utamaduni wa kutoadhibiwa kwa uhalifu dhidi ya wanahabari.

UNESCO inasema kulinda wanahabari si jukumu la serikali pekee, bali ni wajibu wa jamii nzima, kwani mashambulizi dhidi ya wanahabari yanapokosa adhabu, wananchi pia hunyimwa haki ya kupata taarifa na ukweli.