Huku dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Kutoadhibiwa kwa Uhalifu Dhidi ya Waandishi wa Habari, Kenya imeibua wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya wanahabari, huku wahusika wa uhalifu huo wakitajwa kuendelea kutowajibishwa.

Baraza la Habari Kenya (MCK) limesema limerekodi visa 47 vya ukiukaji wa haki za wanahabari kati ya Julai na Septemba, 2026, hali inayodhihirisha mazingira yanayozidi kuwa hatari kwa wanahabari nchini.

Akizungumza kuhusu ripoti ya ukiukaji wa uhuru wa vyombo vya habari nchini, Meneja wa Uhuru wa Vyombo vya Habari na Utetezi wa MCK, Rebecca Mutiso, amesema visa hivyo vinajumuisha mashambulizi 34 ya kimwili dhidi ya wanahabari.

Mutiso amesema wanaume 36 na wanawake tisa walikumbwa na ukiukaji huo, huku Nairobi ikiongoza kwa kurekodi visa 13.

Kwa mujibu wa MCK, wahusika wakuu wa mashambulizi hayo ni makundi ya wahuni, yakifuatiwa na polisi waliotajwa katika visa 12 na wanasiasa katika visa vinane.

Hata hivyo, Homa Bay imetajwa kuwa eneo lililoshuhudia mashambulizi makali zaidi dhidi ya wanahabari katika kipindi hicho.

Mutiso amesema hali hiyo inazua hofu zaidi ikilinganishwa na miaka iliyopita, ambapo visa 17 vilirekodiwa katika kipindi kama hicho mwaka uliopita na 24 mwaka mmoja kabla yake.

Ameonya kuwa ongezeko hilo linaweza kuwa ishara ya hatari zaidi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027, akisema baadhi ya wanahabari tayari wanatafakari kujiondoa katika kazi ya kuripoti uchaguzi kutokana na vitisho vinavyowakabili.

Kenya imeimarika hadi nafasi ya 106 katika orodha ya kimataifa ya uhuru wa vyombo vya habari ya Reporters Without Borders mwaka 2026, kutoka nafasi ya 117 mwaka 2025.

Hata hivyo, MCK imesema mafanikio hayo ya kimataifa hayawezi kuwa na maana ikiwa wahusika wa mashambulizi dhidi ya wanahabari wataendelea kukwepa adhabu.

Ripoti hiyo inaibuka wakati Umoja wa Mataifa ukisisitiza umuhimu wa kuwajibishwa kwa wahusika wa uhalifu dhidi ya wanahabari duniani, huku UNESCO ikionya kuwa asilimia 86 ya mauaji ya wanahabari bado hayapati haki.

MCK imetoa wito kwa serikali, vyombo vya usalama na wadau wengine kushirikiana kuhakikisha wanahabari wanalindwa, mashambulizi yanachunguzwa na wahusika wanachukuliwa hatua za kisheria.

Baraza hilo limesisitiza kuwa kulinda wanahabari ni kulinda haki ya wananchi kupata taarifa, uwajibikaji wa viongozi na demokrasia nchini.