Familia ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, imeamua kuahirisha mazishi ya kaka yao, Wakili Alute Lissu Mughwai, hadi baada ya kutolewa kwa hukumu ya kesi ya uhaini inayomkabili mwanasiasa huyo.

Uamuzi huo umefikiwa kwa lengo la kuwawezesha wanafamilia kushiriki katika usomaji wa hukumu ya kesi ya Tundu Lissu, inayotarajiwa kutolewa Ijumaa, Novemba 6, 2026, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kwa niaba ya familia, Dkt. Vincent Lissu Mughwai amesema mazishi ya marehemu yanatarajiwa kufanyika mkoani Singida, lakini tarehe rasmi itatangazwa baada ya hukumu ya kesi ya ndugu yao kutolewa.

Amesema familia imekubaliana kusogeza mbele shughuli za mazishi ili ndugu na jamaa waweze kuhudhuria mahakamani kusikiliza hukumu hiyo kabla ya kuelekea Singida kwa shughuli za mwisho za kumuaga marehemu.

Katika hatua hiyo, familia imeeleza matumaini yake kuwa Tundu Lissu ataachiwa huru na kupata nafasi ya kushiriki katika mazishi ya kaka yake, ambaye alikuwa mtu muhimu katika maisha yake.

Mughwai alifariki dunia Jumapili, Novemba 1, 2026, majira ya saa nane usiku katika Hospitali ya Selian mkoani Arusha, baada ya hali yake ya kiafya kuzorota kufuatia kuugua kwa muda mrefu.

Kifo chake kimeacha pengo kubwa katika familia ya Lissu, kutokana na nafasi aliyokuwa nayo kama msemaji wa familia na mmoja wa viongozi wakuu wa ukoo.

Mazishi yanatarajiwa kufanyika katika kijiji cha Mahambe, Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida, ambako ndiko nyumbani kwa familia hiyo.

Aidha, marehemu Alute alikuwa wakili wa muda mrefu na mtu aliyekuwa na ushawishi mkubwa katika familia, akitajwa kuwa mfano wa kuigwa na ndugu zake, akiwemo Tundu Lissu.

Ndugu wa marehemu wamesema Alute alikuwa amekuwa akiugua tangu mwaka 1999, huku akipambana na maradhi hayo kwa miaka mingi kabla ya kufariki dunia akiwa na umri wa miaka 72.

Kabla ya kifo chake, marehemu aliwausia ndugu zake kuendeleza upendo, umoja na mshikamano wa kifamilia pamoja na kuendeleza mema aliyokuwa ameyaanzisha.

Kwa upande wake, Chadema imesema itashirikiana na familia katika kipindi hiki cha maombolezo na maandalizi ya mazishi, huku ikisubiri hukumu ya kesi ya Lissu.

Hukumu hiyo inatarajiwa kuwa na uzito mkubwa kwa familia, ambayo imekuwa ikifuatilia kwa karibu kesi hiyo tangu Lissu alipokamatwa Aprili 2025.