Serikali ya Uingereza imeeleza kusikitishwa na kutiwa hatiani kwa Kiongozi wa Upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu, kwa makosa ya uchochezi, huku ikiitaka Serikali ya Tanzania kuzingatia misingi ya haki, uhuru wa kujieleza na utawala wa sheria.
Aidha, Uingereza imetoa wito kwa mamlaka za Tanzania kuimarisha maridhiano ya kisiasa kufuatia uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, ikisisitiza umuhimu wa kujenga mazingira ya kidemokrasia yanayoheshimu haki za binadamu na uhuru wa kisiasa.
Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa Novemba 10, 2026, Waziri wa Uingereza anayehusika na masuala ya Afrika na Maendeleo ya Kimataifa, Kirsty McNeill, amekumbusha kuhusu matokeo ya Kikundi Kazi cha Umoja wa Mataifa kuhusu Ufungaji Holela (UN Working Group on Arbitrary Detention), kilichohitimisha kuwa kuzuiliwa kwa Lissu kulikosa msingi wa kisheria na kukiuka haki za binadamu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyochapishwa kupitia ukurasa rasmi wa Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania, nchi hiyo imesisitiza umuhimu wa Serikali kutekeleza ahadi zake za maridhiano ili kuponya majeraha yaliyotokana na ghasia za uchaguzi uliopita.
McNeill amehimiza Tanzania kuhakikisha mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi unaimarishwa, huku akisisitiza kuwa kesi za kisheria zinapaswa kuendeshwa kwa uwazi, haki na usawa mbele ya sheria.
Kauli hiyo ya Uingereza imekuja siku chache baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, kumwachilia huru Lissu Novemba 6, 2026, katika shtaka la uhaini, lakini ikamtia hatiani kwa kosa mbadala la uchochezi na kumhukumu kifungo cha miaka minne jela.
Hukumu hiyo imeendelea kuzua mijadala kuhusu haki za kisiasa, uhuru wa kujieleza na nafasi ya upinzani katika demokrasia ya Tanzania, huku wito wa maridhiano ukiendelea kutolewa na wadau mbalimbali wa kimataifa.
Uingereza imesisitiza kuwa kuheshimiwa kwa haki za binadamu, utawala wa sheria na uwepo wa mazingira huru ya kisiasa ni muhimu katika kujenga imani ya wananchi kwa taasisi za umma na kuimarisha utulivu wa taifa.
Hata hivyo,baada ya hukumu hiyo,Tundu Lissu alionesha nia ya kutaka kukata rufaa ya dhamana ili kesi yake ifanyike akiwa nje ya gereza.









