Marekani imeiorodhesha Uganda miongoni mwa mataifa 23 duniani yanayotajwa kuwa hatari zaidi kwa raia wake wanaopanga kusafiri nje ya nchi, huku ikiendelea kutoa onyo kali dhidi ya safari za kuelekea taifa hilo la Afrika Mashariki.

Katika tahadhari iliyotolewa Jumatatu, Novemba 9, 2026, Idara ya Mambo ya Nje ya Marekani kupitia kitengo chake cha masuala ya kibalozi imewaonya raia wake kutosafiri Uganda kwa sababu yoyote, ikiashiria uwepo wa hatari zinazohusiana na usalama, afya, ugaidi na machafuko ya kiraia.

Uganda imeorodheshwa katika kundi la nne, Level 4, ambalo ndilo daraja la juu zaidi katika mfumo wa tahadhari za usafiri wa Marekani, likimaanisha “Usisafiri”.

Nchi hiyo imeorodheshwa pamoja na mataifa mengine kama Somalia, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Sudan, Urusi, Iran, Afghanistan na Korea Kaskazini.

Kwa mujibu wa serikali ya Marekani, tahadhari hiyo inatolewa katika maeneo ambako hali ya usalama inaweza kuhatarisha maisha ya wasafiri au ambako serikali yake ina uwezo mdogo wa kutoa msaada wa dharura kwa raia wake.

Marekani imetaja uhalifu, ugaidi, machafuko ya kisiasa na changamoto za kiafya kuwa miongoni mwa sababu kuu zinazochangia Uganda kuendelea kuwa katika kiwango hicho cha tahadhari.

Tahadhari hiyo pia inatokana na uwezekano wa mashambulizi ya kigaidi katika maeneo ya umma, yakiwemo shule, vituo vya usafiri, majengo ya serikali, vituo vya polisi, maeneo ya ibada na vivutio vya utalii kama mbuga za wanyama.

Marekani imeonya kuwa maandamano ya kisiasa yanaweza kuzuka bila taarifa ya mapema, hasa wakati wa mijadala ya kisiasa na shughuli zinazohusiana na uchaguzi.

Aidha, serikali hiyo imeeleza kuwa uwezo wake wa kutoa msaada wa dharura kwa raia wa Marekani walioko Uganda umeathiriwa na changamoto za kiafya zinazohusiana na mlipuko wa Ebola.

Uganda iliwekwa katika kiwango cha nne cha tahadhari Mei 17, 2026, baada ya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola wa aina ya Bundibugyo katika eneo la Ituri nchini DRC. Tahadhari hiyo iliendelea katika mapitio yaliyofanywa Juni 4, 2026.

Marekani pia imeeleza wasiwasi kuhusu uwezo wa polisi wa Uganda kukabiliana na uhalifu mkubwa kutokana na changamoto za rasilimali.

Katika masuala ya usafiri, raia wa Marekani wameonywa dhidi ya kutumia barabara kuu nyakati za usiku kutokana na hatari ya ajali.

Takwimu zilizotajwa katika tahadhari hiyo zinaonyesha kuwa watu 25,808 walihusika katika ajali za barabarani nchini Uganda mwaka 2024, huku 5,144 wakifariki.

Barabara inayounganisha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe na Kampala pia imetajwa kuwa miongoni mwa njia zinazohitaji tahadhari kubwa wakati wa usiku.

Kwa mujibu wa Marekani, wafanyakazi wake wa ubalozi wamepigwa marufuku kuendesha magari nje ya miji mikubwa wakati wa usiku, isipokuwa katika barabara ya Entebe