Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) imeingia katika mvutano na wabunge kuhusu mamlaka ya kusimamia na kuidhinisha kanuni mpya za matumizi ya fedha za kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2027.
Mvutano huo ulijitokeza wakati Mwenyekiti wa IEBC, Erastus Edung Ethekon, alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zinazoongozwa na Mbunge wa Ainabkoi, Samuel Chepkong’a, kujibu maswali kuhusu kanuni za ufadhili wa kampeni za uchaguzi za mwaka 2026.
Wabunge wanasisitiza kuwa Bunge lina mamlaka ya kikatiba kupitia kanuni hizo, kuzifanyia marekebisho au kuzikataa kabla hazijaanza kutekelezwa.
Hata hivyo, Ethekon alisisitiza kuwa IEBC ina mamlaka huru ya kikatiba ya kuweka na kutekeleza viwango vya matumizi ya fedha za kampeni bila kuhitaji idhini ya Bunge.
Chepkong’a aliikosoa tume hiyo kwa kushindwa kuwasilisha kanuni hizo kwa Bunge kabla ya kuzitangaza rasmi katika gazeti la serikali mnamo Agosti 7, 2026.
Alisema masuala yote yanayohusiana na utungaji wa sheria yanapaswa kufuata taratibu za kikatiba, akirejelea Ibara ya 94(5) ya Katiba inayolipa Bunge mamlaka ya kutunga sheria.
Kwa upande wake, Ethekon alieleza kuwa suala hilo tayari limeamuliwa na mahakama, akisema sheria iliyopo haitoi sharti la Bunge kuidhinisha kanuni hizo kabla ya kuchapishwa.
Alirejelea uamuzi wa Mahakama Kuu uliobatilisha kipengele cha Sheria ya Ufadhili wa Kampeni za Uchaguzi kilichotaka kanuni hizo kuidhinishwa na Bunge kabla ya kuchapishwa rasmi.
Kanuni hizo mpya zinaweka viwango vya juu vya fedha ambazo wagombea na vyama vya kisiasa vinaweza kutumia katika kampeni zao.
Kwa mfano, mgombea urais ameruhusiwa kutumia hadi shilingi bilioni 6.11, huku vyama vya kisiasa vikiwekewa kikomo cha matumizi ya shilingi bilioni 24.45.
Wagombea ubunge wanaruhusiwa kutumia kati ya shilingi milioni 15 na milioni 100 kutegemea ukubwa wa maeneo wanayowania, huku wagombea wa viti vya MCA wakiwekewa viwango vya kati ya shilingi milioni 3.48 na milioni 22.09.
Kanuni hizo pia zinataka wagombea na vyama vya kisiasa kufungua akaunti maalumu za benki kwa ajili ya fedha za kampeni, kutunza kumbukumbu za michango na kuwasilisha ripoti za mapato na matumizi yao kwa IEBC.
Michango inayozidi shilingi 20,000 katika harambee za kuchangisha fedha za kampeni pia italazimika kutolewa stakabadhi, huku matumizi yanayozidi shilingi milioni moja yakihitaji ripoti ya ukaguzi wa hesabu.
Hata hivyo, utekelezaji wa kanuni hizo umesimamishwa kwa muda na Mahakama Kuu kufuatia kesi iliyowasilishwa kupinga baadhi ya vipengele vyake.
Mvutano huo unazua maswali kuhusu namna Kenya itakavyodhibiti matumizi ya fedha katika uchaguzi ujao, hasa wakati ambapo gharama za kampeni na ushawishi wa wafadhili wakubwa vinaendelea kuwa masuala muhimu katika ushindani wa kisiasa.
Hadi sasa, kanuni hizo zinasubiri mwelekeo wa kisheria huku maandalizi ya uchaguzi wa 2027,ukiendelea.









