Mhubiri wa injili nchini Kenya ameamriwa kulipa aliyekuwa mkewe fidia ya Sh900,000 baada ya kupatikana na hatia ya kufichua hali yake ya maambukizi ya virusi vya HIV bila ridhaa yake, hatua iliyomsababishia madhara ya kisaikolojia na kuvunjiwa heshima.

Hukumu hiyo imetolewa na Mahakama ya "HIV na AIDS Tribunal," ambayo ilibaini kuwa mwanamume huyo alikiuka sheria inayolinda usiri wa taarifa za afya za watu wanaoishi na VVU kwa kusambaza taarifa za hali ya mkewe kwa watu wengine.

Mwanamke huyo, aliyetajwa kwa jina la kificho LGG, aliwasilisha kesi dhidi ya aliyekuwa mumewe GMM Mei 25, 2026, akimtuhumu kufichua hali yake ya kiafya kwa jamaa, watu wa kanisa na wanajamii bila idhini yake.

Katika kesi hiyo, mwanamke huyo alisema ndoa yao ilizaa watoto watatu kabla ya kutengana na kuachana rasmi mwaka 2016.

Alieleza kuwa matatizo katika ndoa yao yaliongezeka baada ya kugundulika kuwa ana VVU, akidai kuwa mumewe alianza kumdhalilisha na kumtishia kutompa fedha wala mali kutokana na hali yake ya kiafya.

Aidha, alidai kuwa aliyekuwa mumewe alitumia taarifa hizo kumfedhehesha wakati wa migogoro yao ya kifamilia, huku akisema kufichuliwa kwa hali yake kulimletea unyanyapaa, maumivu ya kihisia na kuathiri afya yake ya kisaikolojia.

Mwanamke huyo aliwasilisha mashahidi watatu, wakiwemo jirani, mshiriki wa kanisa na dada yake, ambao walitoa ushahidi kuhusu madai ya kufichuliwa kwa hali yake.

Jirani alieleza kuwa alimsikia mwanamume huyo akimwambia mwanamke huyo kwa lugha ya Kikuyu kuwa ana VVU, huku akidai kuwa taarifa hizo zilisambazwa pia kwa watu wengine katika jamii.

Katika utetezi wake, mhubiri huyo alikanusha madai hayo, akisema alikuwa akimsaidia aliyekuwa mkewe baada ya kujua hali yake na kwamba walihudhuria ushauri nasaha wa wanandoa kwa takriban miaka miwili.

Mwanamume huyo pia alidai kuwa migogoro yao ilikuwa ya ndoa na haikuhusiana na hali ya kiafya ya aliyekuwa mkewe.

Katika uamuzi wake, Tribunal ilibaini kuwa baadhi ya madai ya kufichuliwa kwa hali ya mwanamke huyo yalithibitishwa, ingawa ilitupilia mbali madai kuhusu kufichuliwa kwa taarifa hizo kanisani kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha.

Mahakama hiyo iliamua kuwa kufichua hali ya VVU ya mtu bila ridhaa yake ya maandishi ni ukiukaji wa sheria, na kumwamuru mhubiri huyo kulipa Sh500,000 kwa kufichua taarifa hizo na Sh400,000 kwa madhara ya kisaikolojia.

Aidha, alizuiwa kisheria kuendelea kufichua hali ya afya ya aliyekuwa mkewe kwa watu wengine.

Uamuzi huo unaangazia umuhimu wa kulinda faragha ya watu wanaoishi na VVU na kupinga unyanyapaa unaoweza kuathiri maisha yao katika familia na jamii.