Serikali imeanzisha mikakati mipya ya kuwatafuta maelfu ya Wakenya ambao vitambulisho vyao vya kitaifa vimekamilika lakini hawajavichukua, huku ikiharakisha zoezi hilo kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Katibu Mkuu katika Idara ya Uhamiaji na Huduma za Raia, Dkt. Belio Kipsang, amesema jumla ya vitambulisho 557,930 bado vinasubiriwa kuchukuliwa katika vituo mbalimbali vya usajili nchini, huku karibu 400,000 vikiwa vimekwama kwa zaidi ya miaka 10.
Akizungumza mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Utawala na Usalama wa Ndani Alhamisi, Novemba 5, 2026, Kipsang alisema serikali imewashirikisha machifu na manaibu wao katika kuwatafuta wamiliki wa vitambulisho hivyo katika maeneo yao.
Chini ya mpango huo, maafisa wa utawala wa serikali ya kitaifa watapewa orodha ya vitambulisho ambavyo havijachukuliwa ili kuwasaidia kuwafikia wahusika na kuhakikisha wanavipata kabla ya kuanza kwa usajili wa wapiga kura Januari 2027.
Serikali pia inakamilisha mfumo wa kielektroniki kupitia jukwaa la e-Citizen utakaowezesha waombaji kupokea ujumbe mfupi wa simu mara tu vitambulisho vyao vinapokuwa tayari kuchukuliwa.
Aidha, Idara ya Uhamiaji inazingatia kuruhusu wazazi, walezi na watu wengine walioidhinishwa kuchukua vitambulisho kwa niaba ya wamiliki, baada ya kufanyika kwa ukaguzi wa kutosha kuthibitisha utambulisho wao.
Kipsang alisema serikali imeondoa ada zote za kupata vitambulisho vipya na kuvibadilisha, ikiwemo Shilingi 300 zilizokuwa zikitozwa kwa vitambulisho vipya na Shilingi 1,000 kwa vile vya kubadilisha.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge walielezea wasiwasi kuhusu ucheleweshaji wa kupokea vitambulisho katika maeneo mbalimbali, licha ya serikali kuwekeza katika teknolojia ya kisasa.
Mbunge wa Teso Kusini, Uku Kaunya, alisema zaidi ya vitambulisho 5,000 katika eneo la Amagoro vimechelewa kufikishwa katika vituo vya usajili kwa muda wa miezi miwili hadi mitatu.
Kwa upande wake, Kipsang alisema idara hiyo ina uwezo wa kuchapisha vitambulisho 20,000 kila siku na inalenga kuhakikisha maombi yanashughulikiwa na nyaraka kufikishwa kwa wahusika ndani ya siku saba hadi 10.
Alitaja Kaunti ya Busia kuwa na vitambulisho 11,000 vilivyochakatwa katika siku 30 zilizotangulia, huku Kericho ikiwa na vingine 17,000 vinavyoendelea kushughulikiwa.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Gabriel Tongoyo, alimtaka Kipsang kuchunguza malalamishi ya wabunge kuhusu ucheleweshaji katika maeneo yao na kuchukua hatua zinazofaa.
Aidha, Kipsang alifafanua kuwa tarehe za mwisho wa matumizi zinazowekwa kwenye vitambulisho vipya zinahusu teknolojia na taarifa zilizohifadhiwa kwenye chipu, wala si uraia wa mwenye kitambulisho.









