Mahakama Kuu ya Tanzania imetangaza kuwa sheria zilizokuwa zikiruhusu walimu kuwachapa wanafunzi shuleni zinakiuka Katiba, katika uamuzi unaotajwa kuwa ushindi mkubwa kwa haki za watoto nchini humo.
Uamuzi huo ulitolewa Novemba 3, 2026, na jopo la majaji watatu, Amir Mruma, Hassan na Irene Musokwa, ambao walibatilisha vifungu vitatu vya kanuni za elimu zilizokuwa zikiruhusu adhabu ya viboko kwa wanafunzi.
Mahakama ilibaini kuwa Kanuni za 2, 3 na 6 za Education (Corporal Punishment) Regulations, Government Notice No. 294 of 2002, zinakiuka vifungu vya Katiba vinavyolinda utu wa binadamu na kupiga marufuku mateso pamoja na adhabu za kikatili, zisizo za kibinadamu au zinazodhalilisha.
Kesi hiyo ilifunguliwa mwaka 2025 na Samweli Maduhu Mangu dhidi ya Waziri wa Elimu, kufuatia kifo cha mwanafunzi Mhoja Maduhu mnamo Machi 2025.
Kabla ya uamuzi huo, kanuni zilizokuwa zikifanya kazi ziliruhusu walimu kutoa adhabu ya viboko katika mazingira fulani, ikiwemo makosa makubwa ya kinidhamu.
Kanuni hizo ziliweka masharti ya namna adhabu hiyo ilivyopaswa kutekelezwa, zikiwemo kuzingatia uzito wa kosa, umri, jinsia na hali ya afya ya mwanafunzi, huku zikizuia viboko visizidi vinne kwa tukio moja.
Hata hivyo, mahakama ilibaini kuwa masharti hayo hayawezi kuhalalisha kitendo kinachokiuka haki za kikatiba za watoto.
Uamuzi huo umeibua wito kwa serikali kupitia upya sheria na kanuni zinazohusu nidhamu shuleni ili kuhakikisha kuwa zinazingatia haki, usalama na utu wa wanafunzi.
Wadau wa haki za watoto wameitaka serikali kuondoa kabisa vifungu vinavyoruhusu adhabu ya viboko na kuweka mfumo wa nidhamu unaotumia njia zisizo za kikatili.
Mratibu wa Taifa wa Women in Law and Development in Africa, Anna Kulaya, amesema adhabu ya viboko haijasaidia kuboresha tabia za wanafunzi, bali inaweza kuwafanya kuwa wakaidi zaidi.
Amependekeza shule kutumia mbinu za kujenga tabia, ikiwemo kuwapa wanafunzi kazi za ziada za kitaaluma na shughuli za kuwajibika kwa mazingira ya shule.
Hata hivyo, wadau wamesisitiza kuwa utekelezaji wa uamuzi huo unahitaji mabadiliko ya sheria na ushirikiano kati ya serikali, walimu, wazazi na mashirika ya kutetea haki za watoto.









